
MWANASIASA anayechipukia, Nuru Okanga amedai kwamba yeye kama mmoja wa wakereketwa wa sera za kinara wa ODM, Raila Odinga amebaki katika njia panda baada ya kiongozi huyo kuingia katika ubia na rais Ruto.
Okanga anahisi kwamba
Odinga kukubali ODM kufanya kazi na chama tawala cha UDA kumewaacha wafuasi
wake wengi katika hali ya kuchanganyikiwa.
“Mimi ni mtu wa Raila
Odinga na nakubaliana na hilo, lakini Baba kwa kweli anatuchanganya. Juzi akiwa
katika mazishi huko Mlima Kenya alisema kuwa hayuko kwa serikali. Sasa lini
ndio lipi? ako wapi?” Okanga alisema.
Licha ya kukiri
kuchanganyikiwa na hatua hiyo, Okanga alisema mkubwa haulizwi swali na kudai
kwamba kwa wale wanaojua siasa za kinara huyo, wanajua kwamba kuungana kwake na
serikali ni moja ya mbinu za kufifisha ushawishi wa chama tawala, UDA.
Alitolea mfano jinsi
Odinga aliunmgana na hayati Moi mwaka wa 1999 na miaka miwili baadae kuelekea
uchaguzi wa 2002, alikififisha chana cha KANU kwa kuondoka na kila mtu na
kutangaza ‘Kibaki tosha’.
Okanga alitabiri kwamba
Odinga atafanya vivyo hivyo kwani ataondoka na kila mwishoni mwa 2026 na kuacha
UDA kikiwa bila ushawishi wowote wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027.
“Tumemuachia hiyo nafasi,
wacha acheze huo mpira, na tunajua Baba venye anacheza siasa yake sababu yeye
aliua KANU. Hiki chama cha UDA hakuna mahali kinaenda. Baba atatoka na timu
yote 2026 ikikaribia mwisho tukikaribia uchaguzi,” Okanga alidai.
Mwezi jana, Odinga alitia
saini ya ubia mpya kati ya chama cha ODM na UDA katika kile alichokisema kwamba
ni hatua ya kutuliza joto la siasa humu nchini ili kutoa nafasi kwa rais
kufanya kazi.
Ni ubia ambao Ruto
amekuwa akiupigia debe katika ziara zake Maeneo mbalimbali akisema kwamba ni
hatua nzuri ambayo itaona Maeneo mengi yakipokea maendeleo kwani hakutakuwa na
siasa.
Ambacho kila mtu
anasubiria ni je, ubia kati ya Odinga na Ruto utadumu kwa muda upi?