
MCA mtarajiwa wa wadi ya Kholera, Nuru Okanga amedai kwamba atakuwa MCA wa kwanza humu nchini kuwasilisha mswada wa kutaka kupunguzwa kwa mishahara ya MCAs.
Okanga, ambaye amekuwa
akiweka matumaini yake hai ya kuchaguliwa kama MCA katika kaunti ya Kakamega
katika uchaguzi mkuu ujao wa 2027, alisema kwamba MCAs hawafai kuwa na
mishahara mikubwa kwani kazi nyingi kwenye kaunti hufanywa na magavana.
Alisema kuwa ikiwa
atachaguliwa, wiki ya kwanza ofisini itakuwa ya kutayarisha mswada wa
kupunguzwa kwa mishahara ya wawakilishi wadi, huku akiwasuta kwa kutaka
nyongeza zaidi.
“Juzi nimeona MCAs
wakisema eti wanataka waongezewe mishahara, ya kazi gani? kununua magari
makubwa makubwa? Kwanza nataka mimi nikiwa MCA, nikichaguliwa hivi pap,
napeleka mswada kwa bunge, mshahara wa MCA upunguzwe,” Okanga alifoka.
“Urudi chini! Kwa sababu
MCA ni kazi gani anafanya? Kazi nyingi kaunti ndio inafanya kutoka kwa kulima
barabara, hadi vitu vingine. Hivyo MCAs wanafaa watuambie, kwanza mimi
nikichaguliwa nitapeleka miswada kali kali kwa bunge,” aliongeza.
Akihojiwa iwapo hatua
hiyo haitamsababishia chuki kutoka kwa viongozi wenzake, Okanga alisema kwamba
masilahi yake yatakuwa kwa wananchi na si kwa viongozi wenzake.
‘Mimi nitakuwa n a
masilahi ya watu wangu, wewe kiongozi nichukie lakini kwa ground niko sawa.
Mimi nafuata ground, sifuati kiongozi. Na ground ndio imeniweka hapo. Watu
wamefeli kwa sababu wamefuata viongozi. Mimi nikichaguliwa nitakaa na watu wa
chini,” alisema huku akitolea mfano wa jinsi mbunge Peter
Salasya anatangamana na wananchi.
Kauli yake kuhusu
kupunguzwa kwa mishahara ya MCAs inakuja wiki chache baada ya MCAs katika
kongamano lao Nairobi kudai nyongeza ya hadi 700% ya mishahara.
Wakizungumza katika siku
ya mwisho ya Mkutano wa 5 wa Bunge la Kaunti jijini Nairobi, wabunge hao pia
waliazimia kushinikiza kutekelezwa kwa Hazina ya Maendeleo ya Wadi na uhuru wa
kifedha kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Kaunti, wakisema kuwa hatua hizi ni muhimu
kwa uangalizi mzuri na utoaji wa huduma.