
Mwakilishi wa wadi ya Kariobangi North, Joel Munuve, amefariki dunia akiwa anapokea matibabu katika hospitali ya kibinafsi iliyoko barabara ya Kiambu, jijini Nairobi.
Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, Kennedy Ngondi, amethibitisha kifo hicho, akieleza kuwa Munuve alikuwa njiani kuelekea ofisini katika eneo la jiji kuu (CBD) alipokumbwa na maumivu ya kifua ya ghafla. Alikimbizwa hospitalini lakini akafariki dunia akiwa katika matibabu.
“Baadaye mwili wake ulihamishiwa katika hifadhi ya maiti ya Lee kusubiri upasuaji wa maiti,” Ngondi alisema.
Spika Ngondi alimtaja Munuve kama kiongozi mwenye bidii na aliyekuwa na moyo wa kuwatumikia watu wake kwa kujitolea.
“Uongozi wa Bunge la Kaunti ya Nairobi unasikitika kutangaza kifo cha ghafla cha mheshimiwa Joel Munuve, mwakilishi aliyechaguliwa wa wadi ya Kariobangi North,” alisema.
“Alianguka ghafla na kufariki dunia mapema leo. Munuve alikuwa kiongozi aliyejitolea, mtumishi asiyechoka wa wananchi, na sauti ya shauku ndani ya bunge.”
Ngondi alisifu kujitolea kwa Munuve katika kuhudumia umma, akisema kuwa atakumbukwa kwa heshima na mapenzi makubwa kutoka kwa wale aliowatumikia.
“Kifo chake ni pigo kubwa kwa familia yake, wapiga kura wake, na serikali nzima ya Kaunti ya Jiji la Nairobi. Kwa niaba ya Bunge la Kaunti ya Nairobi, na kwa niaba yangu kama Spika, tunatoa rambirambi zetu za dhati kwa familia, marafiki, na wakazi aliowatumikia,” alisema Ngondi.
Alibainisha kuwa mipango ya mazishi
itatangazwa baadaye.