logo

NOW ON AIR

Listen in Live

RIP: Tasnia ya Reggae yapoteza gwiji mwingine – Max Romeo

Max Romeo amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80 kutokana na matatizo ya moyo.

image
na Samuel Mainajournalist

Mastaa wako14 April 2025 - 09:35

Muhtasari


  • Kwa mujibu wa familia yake, Romeo – ambaye jina lake halisi ni Maxwell Livingston Smith – alifariki Ijumaa katika hospitali iliyoko Saint Andrew Parish, Jamaica.
  • Max ameacha alama isiyofutika katika muziki wa reggae ulimwenguni.

Max Romeo

Mwanamuziki maarufu wa reggae kutoka Jamaica, Max Romeo, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80 kutokana na matatizo ya moyo.

Kifo chake kilithibitishwa kupitia taarifa rasmi iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii Jumapili, na kusababisha wimbi la rambirambi kutoka kwa mashabiki duniani kote.

Kwa mujibu wa familia yake, Romeo – ambaye jina lake halisi ni Maxwell Livingston Smith – alifariki Ijumaa katika hospitali iliyoko Saint Andrew Parish, Jamaica.

 “Kwa huzuni kubwa tunatangaza kifo cha mpendwa wetu Max. Tunashukuru kwa upendo na rambirambi, na tunaomba faragha wakati huu. Mashujaa hawafi kamwe.” Taarifa ya familia ilisomeka.

Binti yake, Azana Smith, alieleza kuwa familia imevunjika moyo na inaomboleza kwa huzuni

“Baba yangu Maxie Smith hayupo tena katika dunia hii, lakini ataendelea kuishi mioyoni mwetu,” alisema kupitia mahojiano na DancehallMag.

Max Romeo alianza muziki miaka ya 1960 kama mwanakundi la Emotions, kabla ya kujitosa katika kazi ya msanii wa kujitegemea.

Mwaka 1968 alitikisa ulimwengu kwa kibao chake "Wet Dream", kilichopigwa marufuku na BBC kutokana na maudhui yake ya wazi ya kimapenzi, lakini kiliibuka kuwa maarufu na kuingia kwenye orodha ya nyimbo bora Uingereza kwa wiki 25.

Mbali na "Wet Dream", Max pia alifahamika kwa nyimbo kama War Ina Babylon na Chase The Devil, ambazo baadaye zilisampuliwa na wanamuziki wengine kama The Prodigy.

Albamu yake ya mwaka 1976, War Ina Babylon, iliyozalishwa na Lee ‘Scratch’ Perry na kundi la The Upsetters, ilimfanya kuwa miongoni mwa magwiji wa reggae wa mtindo wa roots.

Katika maisha yake ya kisiasa na kijamii, wimbo wake Let the Power Fall ulitumiwa katika kampeni ya uchaguzi ya chama cha People's National Party mwaka 1972 chini ya Michael Manley.

Mwaka 2023, Max aliishtaki kampuni ya Universal Music Group na PolyGram Publishing, akidai kutolipwa mirabaha tangu mwaka 1976, ambapo alidai fidia ya dola milioni 15.

Wakili wake, Errol Michael Henry, alimkumbuka kama “mtu mpole, mkarimu, na mwenye upendo mkubwa kwa familia yake.”

Max ameacha alama isiyofutika katika muziki wa reggae ulimwenguni. Hakika, mashabiki wake hawatamsahau kamwe.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved