
KIUNGO wa kati wa Manchester City Kevin De Bruyne ametangaza kuwa ataondoka katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu kufuatia miaka 10 ya kubebea mataji kwenye Uwanja wa Etihad.
De Bruyne, bingwa mara sita wa Premier League akiwa na Man
City, alitangaza uamuzi wake huo katika taarifa ya hisia kwenye mitandao ya
kijamii siku ya Ijumaa.
Mbelgiji huyo amecheza mechi 280 za Premier League kwa
kikosi cha Pep Guardiola, akifunga mabao 70 na kutoa asisti 118 kwenye
mashindano hayo, jumla ya mabao hayo ikiwa ya pili baada ya rekodi ya muda wote
ya Ryan Giggs ya 162.
Katika taarifa yake De Bruyne alisema: "Wapendwa wa Manchester,
ukiona hili, labda unatambua wapi hii inaelekea. Kwa hivyo nitaingia moja kwa
moja na kuwafahamisha kuwa hii itakuwa miezi yangu ya mwisho kama mchezaji wa
Manchester City.”
"Kandanda iliniongoza kwa nyinyi nyote-na kwa jiji hili. Kukimbiza
ndoto yangu, bila kujua kipindi hiki kungebadilisha maisha yangu. Jiji hili.
Klabu hii. Watu hawa ... walinipa KILA KITU. Sikuwa na chaguo ila kurudisha
KILA KITU! Na tafakari hili, tulishinda KILA KITU.”
"Tupende tusipende, ni wakati wa kusema kwaheri. Suri, Rome,
Mason, Michèle, na mimi tunashukuru sana kwa nini eneo hili limemaanisha kwa
familia yetu. 'Manchester' itakuwa kwenye hati za kusafiria za watoto wetu
milele - na muhimu zaidi, katika kila moja ya mioyo yetu. Hii itakuwa NYUMBANI
kwetu daima.”
"Hatuwezi kuwashukuru City, klabu, wafanyakazi, wachezaji wenzetu,
marafiki na familia vya kutosha kwa safari hii ya miaka 10. Kila hadithi inaisha,
lakini hii imekuwa sura bora zaidi. Hebu tufurahie nyakati hizi za mwisho
pamoja! Nawapenda sana, KDB,” barua yake ilisomeka kwa ukamilifu.
Mbali na mataji yake sita ya Ligi Kuu ya England, mchezaji
huyo mwenye umri wa miaka 33 alitawazwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Uingereza
mara mbili, 2019/20 na 2021/22, na pia alishinda tuzo ya Playmaker wa assists
nyingi zaidi katika msimu mara tatu, 2017/18, 2019/20 na 2022/23.