
Kocha mkuu wa Harambee Stars, Benni McCarthy, ametangaza kikosi cha muda kitakachojiandaa kwa Mashindano ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) yanayotarajiwa kufanyika mwaka 2024.
Mashindano haya yanawahusu pekee wachezaji wanaoshiriki ligi za nyumbani katika mataifa yao.
Kikosi hicho kimetokana na wachezaji wa Ligi Kuu ya FKF, kikionyesha vipaji bora vya ndani ya nchi.

Vinara wa safu ya ushambuliaji ni wafungaji bora wa ligi, Moses Shuma, Emmanuel Osoro, na Ryan Ogam, ambao hadi sasa wamefunga mabao 17, 16, na 15 mtawalia msimu huu.
Mshambuliaji wa Sofapaka, Edward Omondi, pia ameitwa kikosini kufuatia msimu mzuri aliokuwa nao katika klabu yake.
Katikati ya uwanja, kiungo wa Kenya Police FC, Mohammed Bajaber, anaongeza ubunifu, huku wachezaji wapya waliopata mwito wa kwanza kujiunga na timu ya taifa wakiwemo Keith Imbali, na wawili wa Ulinzi Stars, Yakeen Muteheli na Staphod Odhiambo.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Kenya kushiriki katika mashindano ya CHAN. Taifa hili lilishiriki mara ya mwisho mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2019, ambapo liliaga mashindano hayo katika hatua ya makundi.
Safari hii, Harambee Stars watakuwa na hamasa ya kufanya vizuri zaidi hasa kutokana na fursa ya kucheza nyumbani. Timu hiyo inatarajiwa kuingia kambini tarehe 10 Julai 2025.
Kenya itaanza kampeni yake ya CHAN 2024 dhidi ya DR Congo mnamo Agosti 3 katika Uwanja wa Kasarani, kabla ya kumenyana na Angola, Morocco, na Zambia katika hatua ya makundi.
Kwa mara ya kwanza katika historia, CHAN itandaliwa kwa pamoja na mataifa ya Kenya, Uganda, na Tanzania.
Mashindano haya yatafanyika kuanzia Agosti 2 hadi Agosti 30, 2025, na yanatarajiwa kuwa sherehe ya kusisimua ya vipaji vya kandanda vya ndani katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Walinda Mlango: Faruk Shikhalo (Bandari), Sebastian Wekesa (Kariobangi Sharks), Brian Opondo (Tusker FC)
Mabeki: Siraj Mohammed (Bandari FC), Manzur Suleiman (KCB), Pamba Swaleh (Bandari FC), Abud Omar (Kenya Police), Alphonce Omija (Gor Mahia), Sylvester Owino (Gor Mahia), Michael Kibwage (Tusker), Daniel Sakari (Kenya Police), Lewis Bandi (AFC Leopards), Kevin Okumu (KCB)
Viungo: Brian Musa (Kenya Police), Kelly Madada (AFC Leopards), Keith Imbali (Shabana), Alpha Onyango (Gor Mahia), Mathias Isogoli (KCB), Staphod Odhiambo (Ulinzi Stars), Austine Odhiambo (Gor Mahia), Ben Stanley (Gor Mahia)
Washambuliaji: Mohammed Bajaber (Kenya Police), Boniface Muchiri (Ulinzi Stars), David Sakwa (Bandari), Emmanuel Osoro (FC Talanta), Yakeen Muteheli (Ulinzi Stars), Edward Omondi (Sofapaka), Ryan Ogam (Tusker), Moses Shummah (Kakamega Homeboyz), Beja Nyamawi (Bandari)