Beki wa zamani wa Manchester United na England Wes Brown ametangazwa kuwa muflisi na Mahakama Kuu, kulingana na ripoti za hivi punde.
Brown, ambaye alipata pauni 50,000 kwa wiki wakati alipokuwa Manchester United, alitangazwa kufilisika Aprili 12 baada ya ombi kuwasilishwa na HMRC mnamo Februari 27 mwaka huu.
Brown, ambaye alianza maisha yake ya soka akiwa na Manchester United kama mchezaji wa akademia, aliichezea klabu hiyo katika mechi zaidi ya 200, na kushinda mataji mengi ya kuvutia ikiwa ni pamoja na Ligi ya Mabingwa mara mbili, mataji matano ya Premier League, mawili ya FA Cup na mawili ya Ligi. Pia aliichezea timu ya taifa ya Uingereza, akicheza mechi 23.
Baada ya kuondoka Manchester United mwaka wa 2011, Brown aliendelea kuchezea klabu za Sunderland, Blackburn Rovers, na Kerala Blasters nchini India, kabla ya kustaafu mwaka wa 2018. Wakati wa kustaafu kwake, alikuwa mchezaji wa mwisho kutoka kwa kikosi cha Manchester United kushinda mataji matatu maarufu Treble-1999.
Kulingana na majarida ya Uingereza, Matatizo ya kifedha ya Brown yalikuja baada ya kuachana na mkewe, Leanne, mwaka jana. Leanne alionekana kwenye kipindi cha uhalisia cha TV cha Real Housewives of Cheshire, na wenzi hao walikuwa wamefunga ndoa katika sherehe ya kifahari mwaka wa 2009. Wana watoto watatu pamoja.
Taarifa za kufilisika kwa Brown zimewashtua mashabiki wengi wa soka wanaomkumbuka kuwa mchezaji aliyefanikiwa na mwenye kipaji. Bado haijulikani ni nini kilisababisha shida za kifedha za Brown au jinsi anapanga kusonga mbele kutoka kwa shida hii huku baadhi wakisema kuwa angefuata ushauri kama wa Hakimi kuandikisha mali yake kwa mamake pengine asingetaabika.
Mapema wiki hii, majarida yaliripoti kwamba Brown sasa anaishi maisha ya taabu ambapo mchezaji wa sasa wa Manchester United Marcus Rashford amejitolea kumpa msaada wa nyumba ya kupanga katika moja ya mali zake mingi.
Kwa mujibu wa Daily Star, Rashford anacheza nafasi yake kwa kumruhusu Brown kukaa katika moja ya nyumba zake za kifahari kwa bei ya chini ya kukodisha. Mshambulizi huyo ni mmoja wa watu kadhaa waliomzunguka Brown, huku Wayne Rooney na Michael Carrick pia wakitoa msaada.
Chanzo kimoja kiliiambia Star: "Inaweza kuonekana kama Wes alikuwa akipata pesa nyingi - kwa watu wengi - lakini shida ni kwamba alikuwa akijaribu kufuata mtindo wa maisha wa wachezaji wenzake kupata pesa mara tano au sita zaidi ya yeye.”