Lamine Yamal dhidi ya 'Godfather' wake Messi kwenye kombe la Finalissima

Fainali ya kombe hilo itachezwa mwaka kesho,2025.

Muhtasari

•Kombe la Finalissima hujumuisha washindi wa kombe la bara Ulaya [Euro ] na washindi wa Copa America.

•Italia na Argentina zilichezwa kwenye fainali ya kwanza kuu,2022 huku Argentina ikishinda Italia 3-0 ugani Wembley.

Image: HISANI

Washindi wa Copa America 2024 Argentina na washindi wa Euro 2024 Uhispania watachuana  kwenye kombe la Finalissima mwaka ujao.

Kombe hili hujumuisha washindi wa mashindano ya kombe la bara Ulaya na washindi wa Copa America.Fainali ya kwanza kabisa au "fainali kuu"  ilichezwa mwaka wa 2022.

Italia na Argentina zilicheza katika fainali ya kwanza kwenye uwanja wa Wembley,huku Argentina ya Lionel Messi ikiibuka kidedea kwa mabao 3-0.

Mwaka ujao, Messi anatarajiwa kuiongoza Argentina tena, wakati huu dhidi ya timu inayochipukia ya Uhispania iliyojaa makinda wenye vipaji akiwemo Lamine Yamal.

Kabla ya pambano la fainali ,Uingereza dhidi ya Uhispania, Yamal aliambia kituo kimoja  cha spoti cha  RAC1  kwamba anatumai Uhispania na Argentina wangeshinda fainali zao ili aweze kukutana na kushindana dhidi ya 'Godfather' wake,Lionel Messi.

"Natumai Messi atashinda Copa América na nitashinda Euro, ili niweze kucheza dhidi yake kwenye Fainali," Yamal alisema.

Hata hivyo ,mambo yalikwenda jinsi Yamal alivyotaka kwani Argentina waliwavuruga Colombia kwenye fainali baada ya kuwapokeza kichapo cha 1-0  huku Uhispania wakiwaonyesha Uingereza ni nani jogoo wa mjini baada ya kuwatia darasani na kuwafunza soka  kwa kichapo cha 2-1 .

Fainali kati ya Argentina na Italia  ilichezwa Juni 1 ,2022  kwa hivyo huenda toleo lijalo likafanyika majira ya joto ya 2025.

Hata hivyo ,fainali hiyo itaadhimisha fainali ya kwanza ya Argentina tangu Ángel Di María kustaafu soka ya kimataifa.

Kabla ya kuanza kwa Copa América 2024, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 36 alitangaza kuwa michuano hiyo itakuwa mara yake ya mwisho kuiwakilisha nchi yake.

Je,Lamine Yamal atampaka tope Lionel Messsi?