
Hali hii kutokana na sheria za Ligi Kuu ya Uingereza zinazohusu wachezaji wa chini ya umri wa miaka 18.
Nwaneri ambaye ana umri wa miaka 17 ameendelea kung'ara katika kikosi cha Arsenal msimu huu, lakini bado anakabiliwa na changamoto ya kutengwa na wachezaji wakubwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Akizungumza kuhusu hali hiyo siku ya Jumanne, Arteta alisema, "Ethan bado hawezi kuwa kwenye chumba chetu cha kubadilishia nguo, jambo ambalo ni la kushangaza. Hata siku za mechi, analazimika kujiandaa sehemu nyingine."
Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu ya England, wachezaji wa chini ya miaka 18 hawaruhusiwi kuwa sehemu ya vyumba vya kubadilishia nguo vya timu za wachezaji wakubwa.
Sheria hii inalenga kuwalinda vijana hao dhidi ya mazingira ambayo yanaweza kuwa magumu kwao.
Hali hii inamaanisha kuwa licha ya mchango wake mkubwa katika timu ya kwanza, Nwaneri hana fursa ya kushiriki moja kwa moja na wachezaji wakubwa katika baadhi ya shughuli za timu, jambo linaloweza kuwa changamoto kwa maendeleo yake.
Hata hivyo, Arteta amesisitiza kuwa klabu inafanya kila iwezalo kuhakikisha kijana huyo anaendelea kukua na kupata usaidizi unaohitajika.
Licha ya kizuizi hicho, Nwaneri ameonyesha kiwango cha juu katika mechi za hivi majuzi. Alikuwa miongoni mwa wachezaji waliovutia katika ushindi wa 5-1 dhidi ya Manchester City, akifunga bao muhimu.
Mbali na kipaji chake, Arteta pia ameeleza kuwa urafiki wa karibu kati ya Nwaneri na mwenzake Myles Lewis-Skelly, ambaye pia ni mzaliwa wa akademi ya Arsenal, umekuwa wa manufaa katika safari yao ya kuzoea mazingira ya kikosi cha kwanza.
"Uhusiano wao ni wa kipekee na unasaidia sana. Wanapitia changamoto pamoja, na hilo linawapa nguvu zaidi," alisema Arteta.
Kwa sasa, Arsenal inabaki kufuata sheria zilizopo huku ikiendelea kulea vipaji vyake chipukizi kwa njia bora.
Ingawa Nwaneri anaweza kukumbana na vikwazo vya kikanuni, uwezo wake wa uwanjani unazidi kuthibitisha kuwa ana nafasi kubwa ya kuwa mmoja wa nyota wa siku zijazo katika soka la Uingereza.