logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Sababu halisi ya Gidi kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha Katibu Mkuu wa Gor Mahia

Gidi amefunguka kuhusu sababu halisi iliyomfanya ajiondoe kwenye kinyang’anyiro cha nafasi ya Katibu Mkuu wa Gor Mahia.

image
na Samuel Mainajournalist

Football24 April 2025 - 08:57

Muhtasari


  • Alisema jina lake halikuwekwa kwenye orodha ya wanachama wa kudumu wa klabu, hali iliyomfanya kutostahiki kuwamo kwenye kinyang’anyiro.
  • Akizungumzia sababu zake za kuwania nafasi hiyo, alisema alitaka kuleta uongozi wa kisasa katika klabu yake anayoipenda.

Mtangazaji wa redio

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi cha Radio Jambo, Joseph Ogidi almaarufu Gidi Gidi, amefunguka kuhusu sababu halisi iliyomfanya ajiondoe kwenye kinyang’anyiro cha nafasi ya Katibu Mkuu wa Gor Mahia mapema mwezi huu.

Akizungumza katika kipindi chake cha asubuhi, mtangazaji huyo maarufu alieleza kuwa uamuzi wake wa kujiondoa ulitokana na changamoto za usajili. Alisema kuwa jina lake halikuwekwa kwenye orodha ya wanachama wa kudumu wa klabu hiyo, hali iliyomfanya kutostahiki kuwamo kwenye kinyang’anyiro.

“Niliwahi kuwania nafasi ya Katibu Mkuu mwaka wa 2016 na nilikuwa katika orodha ya ‘Life Members’ katika timu ya K’Ogallo. Lakini wakati walikuwa wanajumuisha ile Membership List, hawakuweka jina langu. Na sijui ni kwa nini. Nilijaribu kufuatilia wakanieleza kwamba ‘Gidi tulikusahau aje na wewe uko katika orodha ya Life Members?’. Wakati walikuwa wanaweka ile orodha ya mwisho, hawakuweka jina langu. Na orodha ilikuwa inakamilika Machi 30. Kwa hiyo masaa ya kuweka ile orodha ilikuwa imeisha,” Gidi alieleza.

Nyota huyo wa zamani wa muziki alibainisha kuwa alikuwa na chaguo la kwenda mahakamani kujaribu kusimamisha uchaguzi, lakini aliamua kutohujumu mchakato huo.

“Wakati nilikuwa nimetuma ile ombi langu, ile orodha tayari ilikuwa imepelekwa kwa registrar of sports, ambaye tayari alikuwa ameweka muhuri. Kuibadilisha ilikuwa lazima huo mchakato urudiwe tena na siku ya makataa ilikuwa ishaamuliwa pale,” alisema.

“Niliongea na registrar akaniambia hawezi niweke kwenye orodha, labda tu niende kortini niweze kupata court order. Mimi nikajiuliza, imebaki siku mbili tu kabla ya uchaguzi, nikienda kortini nisimamishe uchaguzi wa K’Ogallo ili niwekwe kwenye orodha, nitakuwa nimefanya makossa makubwa sana. Hii ni siku ambayo imewekwa kwa muda na iliamuliwa na mahakama. Mahakama ilikuwa imeamua uchaguzi lazima ufanyike ndani ya siku 90, sasa mimi kama shabiki naende kusimamisha uchaguzi ambao utakuwa ufanyike? Nikasema la hasha, sitaenda mahakamani, wacha nijiondoe,” aliongeza.

Licha ya changamoto hiyo, Gidi alidokeza kuwa hajakata tamaa kuhusu azma yake ya kuongoza Gor Mahia, na huenda akawania nafasi hiyo baadaye.

“Wakati mwingine nikipata nafasi nitaweza kuwania nafasi ya katibu mkuu wa Gor Mahia. Hivyo ndivyo nilijiondoa kwa sababu ya siku ya makataa,” alisema.

Hata hivyo, mtangazaji huyo mahiri alihimiza viongozi wapya kuhakikisha kuwa wanachama wote halali wa klabu wamesajiliwa ipasavyo. Akizungumzia sababu zake za kuwania nafasi hiyo, alisema alitaka kuleta uongozi wa kisasa katika klabu yake anayoipenda.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved