Makamu mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na MipakaIEBC Juliana Cherera amewataka Wakenya kukoma kusambaza picha zake na viongozi wa Azimio la Umoja kwenye mitandao ya kijamii.
Cherera ambaye awali kabla ya kuwa mmoja wa makamishna wa IEBC alikuwa msaidizi wa kibinafsi wa gavana anayeondoka wa Mombasa Ali Hassan Joho alionekana kuchukizwa na hatua ya Wakenya wengi wakipakia picha yake akiwa na Joho katika hali ya ukakasi.
Kamishna huyo ambaye anawaongoza makamishna wengine watatu waliojitenga na matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyotangazwa na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema kwamba ni wakati wakenya wakomae na waache kusambaza picha hizo kwani kipindi hicho alikuwa akitekeleza wajibu wake kwa bosi wake Hassan Joho na hakukuwa na tatizo.
Jumanne baada ya kujikanganya katika takwimu za uchaguzi makamishna hao wanne walipoitisha mkutano na wanahabari katika mgahawa wa Serena, Wakenya wengi walihisi kwamba wanne hao walitumwa na mrengo wa Azimio la Umoja One Kenya ambamo Joho ni mmoja wao ili kuharibia IEBC jina kwa kujitenga na matokeo ya urasi ambayo yalimpa mshindani wao William Ruto ushindi.
Sasa anawataka kuacha kupakia picha hizo na kuwaambia hatua hiyo haitositisha mchakato ambao waliuanzisha wa kuasi matokeo yaliyotangazwa na Chebukati.
“Mimi na wenzangu tumeonyesha ukiukwaji wa taratibu katika mchakato wa kujumlisha kura za Rais. Si haki kubinafsisha masuala. Picha za mimi nikitekeleza majukumu katika nafasi yangu ya awali hazina uhusiano wowote na ukweli tuliouweka wazi,” Juliana Cherera aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko ni mmoja wa watu ambao wamechimbua na kupakia picha kadhaa za Cherera akiwa na viongozi wa Azimio la U moja Kenya Kwanza na haswa aliyekuwa bosi wake Hassan Joho huku akidokeza kwamba hao ndio wajenzi wa hadithi za uongo za kutaka kuipaka IEBC tope kwamba ilimtangaza Ruto kuwa rais mteule kinyume cha sheria.