

Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Kalerwa Salasya amewataka wanawake ambao wamekuwa wakimmezea mate kwenye mitandao ya kijamii kuwa na subira..
Akizungumza wakati wa mahojiano kwenye kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, mwanasiasa huyo kijana aliweka wazi kuwa hapatikani kwa wanawake kwa sasa.
Salasya alibainisha kuwa yuko bize na kazi yake ya ubunge na akaweka wazi kuwa hana haraka ya kutafuta mshirika wa mapenzi.
”Nataka kuwaaambia tuendelee kuwa wapole, tuendelee kuwa watulivu na haya mambo. sababu unaweza kunitamani, lakini hapo kwa kunipata ndo shida,” Salasya alisema.
Mbunge huyo mcheshi alidokeza kuwa ana matamanio makubwa ya kisiasa ambayo ananuia kutimiza, kwa mfano, kuwa rais wa Kenya, na hivyo hana muda wa mahusiano sasa.
“Niko bize sana. Mara niko hapa Nairobi, wakati mwingine niko nyumbani. Niko sijui wapi. Kila wakati nasafiri kutoka mahali moja hadi kwingine hadi niwapange watu wangu wa Mumias Mashariki. Kwa sababu nataka nikuwe rais wa Kenya. Ndio maana nataka niwe nambari moja kwa wabunge wachapakazi nchini Kenya,” alisema.
Salasya aliweka wazi kuwa hayuko tayari kuingia kwenye ndoa kwa sasa akibainisha kuwa kwa sasa anajishughulisha na kufanya kazi kwa wapiga kura wake.
Hata hivyo alidai kuwa amewataka vijana katika eneo la Mumias Mashariki kuoa ili kuzuia uasherati na uhalifu katika eneo hilo.
“Mambo ya ndoa ni mambo ya Mwenyezi Mungu. Niliambia watu wa Mumias Mashariki kwamba wale vijana wote ambao wamebaleghe na kufikisha umri wa kuoa, waoe kwa sababu lazima kila mtu katika eneo bunge awe na majukumu. Wale vijana ambao wanasumbua ni wale ambao hawajaoa,” Salasya alisema.
Mbunge huyo kwa mara ya kwanza alidai kuwa kuoa kwa sasa kunaweza kumfanya apoteze mwelekeo na jukumu kubwa la kuhudumu eneo bunge la Mumias Mashariki ambalo analo.
“Ndio maana nimesema kwamba mimi pekee ndiye nimeruhusiwa katika eneo bunge langu kutooa kwa sasa. Hii ni kwa sababu niko na kazi nyingi. Mimi ni mbunge ambaye nilipata watu wangu wakiwa nyuma sana, na lazima nitengeneze mambo hayo yote,” alisema.
“Nikiingia katika mambo ya wanawake, niingie katika mambo ya kuoa mabibi, nitakosa mwelekeo. Nimesema kwanza nipange eneo bunge, watoto wasome, watoto waanze kushika mwelekeo, nijenge mashule na mabarabara, madaraja, na kila kitu,” aliongeza.
Salasya hata hivyo alifichua kuwa ana mpango wa kuoa angalau wake watatu katika siku za usoni.