logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Najutia kumuua mke wangu - Mwanahabari Moses Dola afunguka kwa uchungu kuhusu kilichojiri

Dola alijawa na hisia kali alipokuwa akisumulia tukio hilo la kusikitisha lililotokea Mei 3, 2011.

image
na Samuel Mainajournalist

Mahojiano09 April 2025 - 16:03

Muhtasari


  • Dola alisema kuwa mkewe alimdunga mkono kwa kutumia makasi kabla yao kuanguka chini, ambapo Wambui alipata jeraha kichwani.
  • Dola alisema kuwa baada ya kugundua kuwa mkewe hakuwa hai, alipoteza fahamu kwa muda kutokana na mshtuko mkubwa.

Moses Dola ndani ya studio za Radio Jambo

Moses Dola, aliyekuwa mwanahabari na ambaye aliachiliwa mwezi uliopita baada ya kutumikia kifungo cha miaka 10 gerezani kwa kosa la kusababisha kifo cha mkewe Sarah Wambui Kabiru bila kukusudia, alijawa na hisia kali alipokuwa akisumulia tukio hilo la kusikitisha lililotokea Mei 3, 2011..

Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na Massawe Japanni, alieleza kuwa mabishano kuhusu sauti ya redio kati yake na mkewe yaligeuka kuwa ugomvi wa kivita, ambao hatimaye ulisababisha kifo cha mama huyo wa mtoto wao mmoja.

Dola alisema kuwa mkewe alimdunga mkono kwa kutumia makasi kabla yao kuanguka chini, ambapo Wambui alipata jeraha kichwani.

“Mimi niling’ang’ana nikachukua ile makasi nikaitupa kitandani. Lakini alipokuwa ananifuata, nikamrukia. Bahati mbaya, akaanguka na akagonga kichwa upande wa kulia. Na hilo likasababisha mauti. Ni jambo ambalo nalijutia sana,” Dola alisimulia.

Mwanahabari huyo wa zamani alieleza kuwa mkewe hakufariki papo hapo, kwani hata alimwambia kwamba alikuwa ameumia kabla yeye (Dola) hajaondoka na mtoto wao.

Alisimulia kuwa baada ya tukio hilo, alikwenda kwa shemeji yake Gitahi kumweleza kuhusu ugomvi huo na kutafuta ushauri. Anasema Gitahi alimshauri atulie na amwache dadake apunguze hasira.

“Kosa kubwa nililofanya ni kwenda kukaa kwa Gitahi badala ya kurudi nyumbani na kumwambia pole halafu tuendelee kunywa. Wakati huo ambapo tulikuwa tunakunywa, Wambui alikuwa anapoteza uhai,” alisema.

Dola alisema kuwa alirudi nyumbani mwake majira ya saa sita mchana, na mfanyakazi wa nyumbani alimwambia kuwa Wambui bado alikuwa chumbani cha kulala,

Alieleza kuwa wakati huo alikuwa ametulia na alikuwa na nia ya kuzungumza na mkewe. Hata hivyo, alipofika chumbani cha kulala alimkuta akiwa hana fahamu.

“Mimi niliingia chumbani nikauliza, ‘Mpenzi, hasira za asubuhi mpaka sasa uko kitandani?’ Wakati huo sikuwa na ile hasira ya asubuhi, nilikuwa tayari kuongea. Nilipomtazama vizuri, ndipo nikaona damu upande wa kulia wa kichwa chake,” Dola alieleza.

 “Mimi huyo, nikaruka kitandani. Nilipomuangalia, hakuwa anasonga. Nikaangalia mapigo ya moyo – yalikuwa sifuri. Nikaangalia shingo, mikono, kifua, katikati ya mapaja – yote yalikuwa sifuri. Ndipo ikanitokea kuwa alikuwa amefariki,” alisema.

Dola alisema kuwa baada ya kugundua kuwa mkewe hakuwa hai, alipoteza fahamu kwa muda kutokana na mshtuko mkubwa.

 “Hapo hapo nikazimia. Nilizimia kabisa. Mshtuko ulikuwa mkubwa sana, nikazimia tu. Nategemea sana ushuhuda wa mfanyakazi kwa sababu ndiye aliyekuwa akiendelea na uchunguzi,” alisema.

Dola alieleza kuwa baada ya kuzinduka, alinuia kwenda kituo cha polisi, lakini alijikuta akiwa Naivasha kabla ya hatimaye kujisalimisha kwa polisi.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved