
Mtangazaji maarufu wa runinga kutoka Uganda, Simon Kaggwa Njala, anayejulikana sana kwa mahojiano yake ya kihistoria ya “Why are you gay?”, ameonyesha mshangao wake jinsi watu bado wanamuhusisha na swali hilo hata baada ya zaidi ya muongo mmoja kupita.
Kupitia chapisho kwenye mtandao wa X mnamo Alhamisi, Machi 27, mtangazaji huyo wa NBS TV alidokeza kuwa, licha ya kuwa na familia, bado anakutana na watu wanaomtania kwa kumwuliza, “Kwa nini wewe ni shoga?”.
Bw Kaggwa, kwa mshangao na kejeli, alihoji kwa nini watu bado wanafikiria hivyo, akisisitiza kuwa ana mke ambaye wamejaliwa watoto naye.
"Ninyi watu, mnanikuta na mke wangu na watoto halafu bado
mnauliza, ‘Kwa nini wewe ni shoga?’ Kwa kweli?" Kaggwa aliandika.
Takriban miaka kumi na mitatu iliyopita, mtangazaji Simon Kaggwa Njala alimkaribisha mwanaharakati wa haki za binadamu wa Uganda Pepe Julian Onziema katika kipindi chake cha Morning Breeze kwenye runinga ya NBS ambapo walikuwa na mahojiano ya wazi kuhusu ushoga nchini Uganda.
Katika mahojiano hayo, Kaggwa alionekana kukerwa na sababu ya mwanaharakati huyo kuchagua kuwa shoga na alitaka sana kuelewa yeye ni nani hasa
"Why are you gay? (Kwa nini wewe ni shoga)?" Kaggwa aliuliza mara kwa mara huku mahojiano yakiendelea.
Onziema ambaye alizaliwa mwanamke hata hivyo hakutaka kuitwa shoga na kusisitiza kuwa yeye ni mwanamume anayevutiwa na wanamke.
"Mimi si mwanaharakati wa haki za binadamu anayetetea usawa kwa watu wenye mtazamo tofauti wa kimapenzi na ujinsia tofauti," alisema
Onziema pia alikiri kuwa na mpenzi mwanamke lakini akaweka wazi kuwa hakuwa akishiriki tendo la ndoa naye.
Alipuuzilia mbali madai kwamba alikuwa akipigia debe ushoga nchini Uganda na akakana kuwa alilipwa kufanya hivyo.
Mahojiano hayo magumu yalikuwa yakiendelea vizuri kabla ya Mchungaji Martin Ssempa ,ambaye ni mkosoaji mkubwa wa wapenzi wa jinsia moja, kuingia studio na kulaani mienendo ya Onziema. Punde baada ya kumuona Bw Ssemoa, mwanaharakati huyo alisimama na kutoka nje lakini alishawishiwa na kurudi baada ya muda mfupi.
Mahojiano hayo ya zaidi ya saa moja yamekuwa gumzo kwenye mitandao
kwa miaka mingi iliyopita huku wanamitandao wakiyarejesha mara kwa mara.