
Kijana wa miaka 20 aliyejitambulisha kama Ryan Kingoi kutoka Ruiru alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mama yake Brigid Wairimu (46) ambaye alikosana naye mwishoni mwa mwaka jana.
Ryan alisema uhusiano wake na mamake uliharibika Disemba baada ya kukataa kazi ambayo mzazi huyo wake alimtafutia na hata kumtusi vibaya.
"Ilikuwa Disemba 16. Nilikuwa nimeteseka na kukosa kazi akaniambia kuna kazi ananitafutia. Alinipigia simu nikiwa kazi. Wakati huo nilikuwa nafanya kazi ya kupika chapati kwa hoteli moja. Vile alinipigia nilicha hiyo kazi nikitumai ile kazi ameniitia ni nzuri. Aliniambia niende Mathare nikakopa pesa nikaenda mpaka Mathare. Mtu ambaye ilikuwa tupatane na yeye ndo niingie kazi kufika simu hashiki.
Mwishowe alinipigia akaniambia ako Uthiru niende mpaka huko. Nikamwambia sina nauli akaanza kuniongelesha vibaya mwishowe akazima simu. Mi kumpigia simu nikapata simu yake ni mteja ikabidi nipigie mama. Kumpigia mama sijui alikuwa kwa moods gani na yeye tena tukakorofishana. Mwishowe nikamuongelesh vibaya tukazozana," Ryan alisimulia.
"Mama alinikasirika kiasi kwamba baadaye alinipigia simu akaniambia nisiwahi kumuita mama yangu na akakata simu. Kumpigia tena akniambia 'enda utafute mama yako. Mimi sio mama yako'. Alikasirika juu nilimwambia aambie yule jamaa alikuwa ananitafutia kazi achukue bibi yake ampeleke kazi ama pia yeye akitaka anaweza enda kufanya hiyo kazi. Nilikuwa chini ya shinikizo. Najuta sana ndio maana nataka kuomba msamaha. Hatujaongeleshana tangu wakti huo. Nimekuwa nikimpigia kutumia simu za marafiki zangu, akiskia ni mimi anakata," aliongeza.
Mamake Ryan alipopigiwa simu alifunguka kwa uchungu masaibu ambayo mwanawe alikuwa amempitisha.
"Nilimwambia aende atafute mama yake na asiwahi kuniita mama. Kuna mambo mengi sio hayo tu. Ni kijana ambaye nimelea pekee yangu kama single mother. Tangu akiwa mdogo nimemlea bila baba yake. Lakini amefika mahali amenidharau kwa sababu ameona amekuwa mtu mzima.
Mimi nilikuwa nimemwambia aishi maisha yake na asinitafute, na asihesabu kama ako na mama. Anihesabie kwa wale wenye mama zao walishakufa. Aishi yake simtaki karibu na mimi," Bi Wairimu alisimulia.
"Nilimfukuza kwangu kwa sababu alikuwa anataka kunipiga. Alinitusi matusi ingine mbaya sana yenye mpaka majirani wanasimama kushangaa. Mpaka wanauliza kama kwa kweli ni mtoto wangu," aliongeza.
Mamake Ryan aliweka wazi kwamba ingawa tayari amemsamehe mwanawe, hako tayari kurejesha uhusiano mzuri naye.
Ryan alisema, "Ningependa anisamehe tuweze kurudiana kwa sababu yeye ndiye alikuwa tegemeo, ni kama back up ya maisha."
Mamake hata hivyo aliendelea kufunguka mengi mazito akieleza jinsi kijana huyo alivyobadilisha mienendo yake baada ya kuanza kutembea na vijana wengine wabaya.
"Mtoto alipatana na makundi. Imagine mtoto akinimbia ati mimi sio mama yake. Eti mtu alimwambia nilimuadopt. Mtoto umebeba miezi sita anaskiza maneno ya watu eti mimi sio mama yake. Alafu anachukua muda wake kuniandikia ujumbe eti 'ninasukuru kwa yale yote umenitendea, na ninashukuru kwa kuniadopt na kunifikisha mahali umenifikisha. Nishagundua wewe sio mama yangu, nakushuru kwa hayo. Asante kwa muda wote umenishughulikia. Hiyo ni nini. Kuna mengi. Kama yeye angejielewa, kuna mengi napitia. Ndio nitamsamehe kama mama. Lakini nimemuachi Mungu ambadilishe," alisema Mama Ryan.
Ryan alidai kwamba ameamua kubadilika na akaomba mamake aweze kumsamehe na kumpokea tena.
Mamake Ryan hata hivyo alisisitiza kwamba anahitaji muda wa kufikiria.
Je, una maoni ama ushauri gani kuhusu Patanisho ya leo?