
Jamaa aliyejitambulisha kama Samba Kakai (29) kutoka kaunti ya Kakamega alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na babake mzazi Soita Kakai (65) ambaye alikosana naye takriban miezi miwili iliyopita.
Samba alisema uhusiano wake na babake uliharibika Disemba mwaka jana baada yay eye kuchukua memory card ya mzazi huyo wake na kuuza.
“Nilichukua memory card ya babangu. Ilikuwa kwa redio. Nilienda nikauza. Ilikuwa tu mimi na yeye kwa hivyo akajua ni mimi. Akaanza kuwa mkali. Nilikubali kwamba ni mimi nilichukua,” Samba alisema.
“Sikuwa na chochote kwa mfuko ndiyo maana niliuza. Tumeongea tu mara moja tangu wakati huo, hakuna kitu alisema,” aliongeza.
Bw Kakai alipopigiwa simu, kijana huyo alichukua fursa kumuomba msamaha na akaahidi kumtafutia memory card nyingine.
“Nakuomba msamaha kwa kuchukua memory card ingine. Nitatafuta ingine nikuletee,” Samba alimwambia babake.
Bw Kakai alisikika kukubali ombi la msamaha la mwanawe na akamtaka amtafutie memory card nyingine haraka.
“Alikuja kunitembelea akatamani, akachukua. Lakini nashukuru ameomba msamaha,” alimwambia mwanawe.
Mzee huyo pia alikuwa na habari za kusikitisha za kumpa mwanawe, “Mwambie pole, ndugu yake alianguka na pikipiki. Atafute tu ingine alete haraka itakuwa sawa.
Pia alimshauri mwanawe kwamba asisite kumuomba chochote akitamani, badala ya kuchukua.
“Ni mtu wa kanisa, anatoka kazi, anakuja kuniibia. Ni mtoto mzuri, ni vizuri ameomba msamaha, mimi sina neno. Mimi ni mzee wa heshima. Nimefanya kazi ya polisi miaka 30, nakula mali yangu polepole. Mtoto akitaka kitu aombe,” Bw Kakai alisema.
Samba alisema ameridhika sana baada ya babake kumsamehe.
Je, una ushauri ama maoni gani kuhusu Patanisho ya leo?