
Bi Esther Akoth (27) kutoka Siaya alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Allan Owino (32) ambaye alikosana naye mwaka jana.
Akoth alisema ndoa yake ya miaka miwili ilisambaratika Machi mwaka jana kufuatia ugomvi wa kinyumbani.
Alisema mumewe alichoshwa na tabia yake ya kutorokea kwao kila walipozozana.
“Tulikuwa tunakosana kwa nyumba. Saa zingine alikuwa ananipiga, saa zingine alikuwa ananifanyia vituko. Akinifanyia hizo vitu nilikuwa naenda kwetu. Ilifika wakati akasema hanitaki juu ya hiyo tabia ya kuenda enda kwetu. Alihama akaenda, nikimpigia simu akawa anakata,” Akoth alisema.
Akoth alisema mumewe alikuwa na tabia ya kutoka nje ya ndoa, na pia alikuwa akimshuku kuwa na mahusiano ya nje.
“Alikuwa anapenda wasichana. Mara nyingi nilikuwa Napata meseji mbaya mbaya kwa simu. Ilifika wakati akawa anatongoza hadi marafiki zangu. Nikimuuliza ananichapa. Ikawa hata mimi anaona kama nafanya umalaya, hadi nikienda ushirika anasema nimeenda umalaya,” alisema.
Aliomba kupatanishwa na baba huyo wa mtoto wake mmoja akieleza kwamba ameshindwa kumtoa moyoni mwake.
“Mi nataka turudiane juu nampenda, naskia siwezi kaa bila yeye. Nimejaribu kukaa bila yeye, lakini naskia nimepoteza mtu muhimu sana katika maisha yangu. Nampenda siwezi kaa bila yeye. Nikijaribu kufuta namba yake najipata naifikiria kila saa, nikilala namuota tu. Nilijaribu kutuma ndugu yangu akasema alikasirika juu ya mimi kuenda enda,” alisema.
Akoth hata hivyo hakupatanishwa na mumewe kwani Allan alikataa kuzungumza kwa simu alipopigiwa.
Katika maneno yake ya mwisho kwa mpenziwe, Akoth alimwambia, “Allan mimi ningependa turudiane, kama kuna makosa nilifanya ikakuudhi nimeacha. Nimeomba msamaha, unisamehe, naona siwezi ishi bila yeye.”