
Wycliffe Ouma (34) kutoka Kisumu alituma ujumbe akiomba
kupatanishwa na aliyekuwa mke wake Stella Ayitso (32) ambaye alikosana naye
takriban miaka saba iliyopita.
Ouma alisema uhusiano wake na Stella uliharibika mwaka wa 2017 wakati mzazi huyo mwenzake alipoenda kusoma katika chuo cha KMTC Kisumu.
Alisema mkewe alianza kubadilika baada ya kuwa shule kwa miezi sita, kabla ya kukatiza uhusiano naye kabisa baada ya muda.
“Tulipatana na yeye 2012. Alikuwa form 4. Alikuwa afanye mtihani
mwaka huo. Tuliongea alirudi baada ya mwezi moja. Aliporudi kwao, aliniambia
ako na mimba. Vile alimaliza mtihani wa kidato cha nne aliogopa kukaa nyumbani.
Aliongea na rafiki yake, wakakuja tukakaa na wao,” Ouma alisimulia.
“Tulikaa mpaka mtoto akafika umri wa kuenda shule. Baada ya mtoto kufikisha miaka mitatu alirudi shule kusoma, alienda KMTC Kisumu. Mimi ndiye nilikuwa nampa nauli anaenda shule. Baada ya kusoma miezi kama sita, alianza kurudia nyumbani baada ya wiki tatu, akaanza kurudi baada ya mwezi mmoja. Hivyo ndivyo alienda kabisa. Wakati huo mtoto alikuwa na mamangu. Alifanya mpango akaenda akachukua mtoto,” aliongeza.
Ouma alidai kwamba dadake Stella alimwambia kuwa mkewe huyo wa zamani tayari ameolewa na Mnigeria ambaye anaishi naye Nairobi.
“Mimi ni Mjaluo na siwezi kuacha mtoto nje. Hiyo ndiyo inaniuma. Ata mimi nilishaoa. Niko na mtoto wa mwaka moja. Stella ashamove on, mimi nataka tu kujua msimamo wa mtoto,” alisema.
Stella alipopigiwa simu, aliweka wazi kwamba tayari amesonga mbele na maisha yake na mtoto anaendelea vyema.
Alisema kwamba amelea mtoto pekee yake n ahata akaibua utata kwamba hana uhakika kuhusu baba mtoto.
“Mimi nilishamove on kitambo sana. Mtoto ako sawa. Hafai kunisumbua kabisa. Nilienda shule, sikumuacha. Alinichukua illegally, mimi nikarudi chuo, nikaendelea. Ilikuwa 2012 baada ya kumaliza shule ya upili, nikazaa nikarudi shule. Mtoto ako na baba mwingine na ako sawa. Mtoto sasa ako na utambulisho mwingine,” Stella alisema.
“Mimi nimelea mtoto pekee yangu. Wewe unajua anakaa aje? Kwetu walikuwa strict sana, nikaamua nyumbani nikawaambia nataka kusoma. Nikapeleka mtoto kwao, wakasema hizo bajeti za shule ni mingi wakashindwa kugharamia. Siko sure kama huyo ndiye babake. Nitakubali afanye DNA. Huyo mtoto ananifanana, na ni kijana,” aliongeza.
Ouma aliweka wazi kwamba ataelekea kortini ili kupata haki ya kumuona mtoto wake. Pia alisema kwamba watafanya DNA.
Stella aliibua madai kwamba hajazungumza na Ouma kwa zaidi ya mwongo mmoja. Pia aliweka wazi kwamba sio rahisi kumpata.
“Kunipata lazima akuwe na connections. Sijaongea na Ouma tangu 2013. Yeye amove on. Amekuwa akinitafuta, mimi sishiki simu zake. Kama atanitafuta ni sawa, lakini saai mtoto ako kwa mikono yangu. Asinitafute ashachoma kabisa,” alisema.
Ouma alimuomba mkewe huyo wa zamani awe anashika simu kila anapompigia.
Je, una ushauri ama maoni gani kuhusu Patanisho ya leo?