
Christine Adhiambo mwenye umri wa miaka 35 kutoka Busia alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Stephen Oduor (35) ambaye amekuwa kwa ndoa naye kwa miaka 16.
Christine alisema hajakuwa na maelewano mazuri na mumewe na akamshtumu kwa kumtekeleza yeye na watoto wao nyumbani na kukwama jijini Nairobi.
"Mume wangu tumeoana miaka 16. Sasa hivi hakuna maelewano. Shida ndogo ndogo tu kwa nyumba zinaleta mvutano. Nataka kujua msimamo wake. Hashughulikii mahitaji ya nyumbani. Nataka tu maelewano mazuri kati yangu naye," Christine alisema.
Mama huyo wa watoto wanne alisema kwamba mara ya mwisho kumuona mumewe ilikuwa mwaka mmoja uliopita wakati alikuwa nyumbani.
"Ameniacha kwa boma yeye ako Nairobi. Nikimpigia, wakati mwingine anashika simu anasema tu Hello kujifanya hakuna network. Wakati mwingine anapatia mtu mwingine ashike.
Kama anaona ni ngumu nijiondoe kwa boma yao ni sawa. Amekaa Nairobi kwa muda. Wakati alikuwa nyumbani mwaka jana ilikuwa tu vita. Tulionana mara ya mwisho mwaka jana mwezi wa tatu," alisema.
Christine alieleza kwamba mumewe amejitenga kabisa na nyumbani na huwa hahudhurii hata shughuli za kifamilia.
"Ndugu zake wakijaribu kuongea naye huwa hashughuliki. Huwa hakuji, ata juzi kulikuwa na matanga kwa boma na hakuja. Huwa naona kichwa yake imekuwa ngumu kwa sababu niko hapo sijaondoka. Niko kwa njia panda kwa sababu wakati mwingine huwa nashangaa nafanya nini hapa," alisema.
Juhudi za kumpatanisha Christine na mumewe hata hivyo hazikufua dafu kwani Bwana Stephen alikosa kushika simu.
Katika ujumbe wake wa mwisho kwa mumewe, Christine alisema, "Stephen nilikuwa nakuomba urudishe mawasiliano juu maswali watoto wananiuliza nashindwa kujibu. Angalau ata tumia watoto wako ujumbe. Lakini kaa ukijua mimi bado nakupenda sana."
Je, una ushauri ama maoni gani kuhusu Patanisho ya leo?