
Mwanadada aliyejitambulisha kama Mercy Kwamboka (25) kutoka Nyamira alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake William Odhiambo (39) ambaye alikosana naye hivi majuzi.
Kwamboka alisema ndoa yake ya miaka miwili iliharibika siku tatu zilizopita kufuatia fitina zilizoibuliwa na jirani ya mama mkwe.
Alisema kuna mama aliyemfikishia mama mkwe ripoti zisizo za kweli ambazo zilisambaratisha uhusiano wake na mumewe.
“Bwanangu alitoka akaenda kazi. Kuna siku nilikuwa naenda kutengeneza simu. Kuenda nikapata huyo fundi hayuko nikaambiwa ako mahali huwa panauzwa pombe. Nikaenda hapo kumtafuta, nikampata, na kulikuwa na mama mwingine kutoka mahali nimeolewa. Huyo mama akakimbia kuenda nyumbani kuambia mama mkwe. Akamwambia ati niko huko juu nimekunywa pombe hadi nimelala, ati akujie mtoto,” Kwamboka alisema.
“Mimi ni fundi nilikuwa natafuta. Mama mkwe alituma mtoto akakuja akapata sijalewa akarudi. Lakini sasa vile aliambiwa hivyo, ata kabla hajajua ashapigia bwana yangu simu akamwambia. Hiyo ikafanya tukakosana na bwana yangu hadi akaniblock. Nikipiga simu inaniambia ako busy,” aliongeza.
Kwamboka alisisitiza kwamba hakubugia pombe ata kidogo, na akadai kwamba mwanamke aliyepeleka ripoti huwa na fitina nyingi. “Sikukunywa ukweli ata kidogo. Bwana yangu akiwa huwa tunakunywa na yeye. Hiyo siku sikukunywa. Huyo mama aliwahi kuleta maneno ingine. Anakuwanga tu na maneno mingi.
Fundi alikuja tu na akanitengezea, na akashughulikia hadi customer wengine. Kutoka juzi bwana wangu ameniweka busy. Mama mkwe hajui Kiswahili nashindwa vile nitaongea na yeye,” alisema.
Kwa bahati mbaya, Kwamboka hakuweza kupatana na mumewe kwani William hakupatikana kwenye simu.
Katika ujumbe wa mwisho, Kwamboka alisema, “Akuje tu nyumbani
afuatilie hiyo maneno ajue kama ni ukweli ama ni uongo.”