
Michael Wekesa mwenye umri wa miaka 41 kutoka Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake Sabina Mwikali (28) ambaye alikosana naye takriban miaka mitatu iliyopita.
Wekesa alisema ndoa yake ya miaka miwili ilivunjika mwaka wa 2022 wakati ambapo alikosana na mkewe kwa kumtusi alipoomba pesa.
“Nilikuwa nakaa na Mwikali Machakos. Tulipatana tukaelewana tukaanza kukaa na yeye. Ikafika mahali akataka kurudi chuo. Alipoenda chuo na mimi nikarudi kwetu Bungoma. Nikiwa Bungoma akaniomba pesa za mahitaji,” Wekesa alisema.
“Wakati huo sikuwa na kazi. Aliomba shilingi elfu mbili kila mwezi. Nikamwambia sina kazi. Yeye akasisitiza nikakasirika na yeye nilimuuliza “kwani anafikiria pesa nachota kwa mchanga”,” aliongeza.
Wekesa alisema anajuta sana kumtusi mama huyo wa mtoto wake mmoja hasa kwa kuwa yeye ni yatima.
“Tuliongea mara ya mwisho kama miezi saba imepita. Ningependa anisamehe ikiwezekana turudiane. Kama amepata mwingine ni sawa,” alisema.
Kwa bahati mbaya, Patanisho hiyo iligonga mwamba kwani kulitokea matatizo ya mawasiliano.
Je, una maoni ama ushauri gani kuhusu Patanisho ya leo?