
Stanlus Okello mwenye umri wa miaka 28 kutoka Mbita, Homa Bay County alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Irene Akoth (28) ambaye alikosana naye mapema mwaka huu.
Okello alisema ndoa yake ya miaka mitatu ilisambaratika Februari mwaka huu wakati ambapo mkewe alimfukuza kwa nyumba kwa kutoshughulikia mahitaji ya boma.
Alisema kwamba masaibu yake ya kifedha yalianza mwaka jana wakati ambapo alichukua mikopo, na pia kujitosa katika mchezo wa Kamari.
“Tulikuwa tunaishi pamoja alafu nilikuwa na mashida. Nilichukua mkopo, dadangu akawa na emergency akaomba Sh250k. Nikachukua mkopo mwingine. Sasa pesa ikawa kidogo kwa sababu nilikuwa nakatwa pesa,” Okello alisimulia.
“Kuanzia Septemba nikalemewa kwa sababu duka nilikuwa nimefungua kutumia mkopo nilienda nikaingia mchezo ya aviator nione kama inaweza ikaleta pesa kidogo nijiboost nayo. Ikanikula vile. Kuanzia hiyo Septemba sikuwa na kitu nikaacha kushughulikia mahitaji. Nikipata kitu kidogo pia wazazi walikuwa wananitegemea juu mimi ndiye firstborn,” aliongeza.
Okello alikiri kwamba mkewe alisaidia kwa mahitaji muhimu ya nyumbani kwa miezi kadhaa hadi Februari mwaka huu ambapo alichoka naye na kumfukuza.
“Mpaka Februari, mke wangu alikuwa ananishikilia mambo kama kodi. Kufikia Februari mke akaniambia hatuwezi endelea hivyo itabidi nimeenda nyumbani nijifikirie. Sikuongea sana nikakubali nikatoka,” alisema.
“Hivi majuzi nimetamani kumuongelesha lakini ameniblock. Aliniambia hataki mambo yangu, nashindwa itakuwaje na tuko na watoto wawili. Saai niko sawa. Sijamaliza kulipa mkopo lakini mambo iko sawa. Sijawahi kumkosea kwa njia nyingine,” aliongeza.
Irene alipopigiwa simu, kwa mshangao alimruka Okello.
“Mimi sijui kama amewadanganya. Mimi simjui,” alisema Irene kisha akakata simu.
Okello alisema, “Ananijua. Itabidi nianze upya.”
"Kulikuwa na stori nyingine ya relatives. Wajomba zangu na mama yangu hawakuwa wanampenda. Walikuwa wanaona kama ni mtu mbaya lakini mimi sikuwa naona ubaya wake,” alisema.
Aliongeza kwamba hakuna haja ya kumtafuta tena mama huyo wa watoto wake wawili na kueleza kuwa Patanisho ilikuwa tegemeo lake la mwisho kurejesha ndoa yake.
“Achana nayo. Nilidhani nitajaribu ya mwisho na nyinyi. Haina haja nimbembeleze sana. Akiamua kurudi ni sawa… Namtakia maisha mema. Kama kuna kitu anahitaji usaidizi kwa watoto asiogope kunipigia simu,” alisema.
Je, una maoni ama ushauri gani kuhusu Patanisho ya leo?