
MWISHONI mwa juma lililopita, Wakenya wa matabaka mbalimbali waliungana na ulimwengu kusherehekea siku ya wapendanao kwa kutunukiana zawadi mbalimbali.
Aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko ni mmoja wa watu
maarufu waliojitokeza kusherehekea siku hiyo kwa njia tofauti ambapo aliamua
kusambaza zawadi kwa watu mitaani.
Sonko ambaye alikuwa ameandamana na timu yake jijini Nairobi
alisambaza zawadi za mandhari ya Valentino zikiwemo maua, divai na vitu vingine
vya kuonyesha mapenzi.
Mhisani huyo aliwashangaza wengi alipoamua pia kujumuisha
mipira ya kushiriki mapenzi katika zawadi zake na kuwapa watu, zawadi ambazo
zilipata mapokezi ya kipekee.
Sonko alipeleka kwenye ukurasa wake wa X akaeleza sababu ya
kusambaza zawadi za aina hiyo, akisema kwamba aliona ni vyema kuwapa watu
mipira ya kujikinga dhidi ya maradhi ya zinaa kwa sababu shirika la Marekani,
USAID ambalo kwa muda mrefu limekuwa likisambaza kondomu kwa watu limesitisha
shughuli zake.
“Tunapoadhimisha Siku ya Wapendanao leo, nilisambaza zawadi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na maua, chokoleti, mvinyo, na hata kondomu za ladha kwa ajili ya kujilinda, kutokana na kwamba USaid haipo nasi tena na imeondoa msaada wake,” Sonko alisema.
USAID ilitangaza kusitisha shughuli zake katika mataifa
kadhaa duniani baada ya rais mpya wa Marekani, Donald Trump kuagiza kukatwa kwa
misaada kwa mataifa ya nje, katika sera yake ya ‘Marekani Kwanza’.