
MWANAMUME ambaye kadi yake ya ATM iliibwa na kutumika kununua tikiti ya mchezo wa bahati nasibu ya kushinda shilingi 67,815,000 ametoa ombi la kipekee kwa wezi hao kujitokeza ili kumgawia kitu kidogo kutokana na ushindi huo.
Wezi hao walinunua kadi ya mwanzo
iliyoshinda ya €500,000 (Sh67,815,000) na kadi hiyo iliyoibwa katika jiji la
Toulouse nchini Ufaransa.
Lakini tikiti haijawasilishwa kudai zawadi.
Mwathiriwa wa wizi huo, aliyetambuliwa
katika hati za polisi kama Jean-David E, mkoba wake uliokuwa na kadi yake ya
benki uliibiwa kutoka kwa gari lake mapema mwezi huu.
Aliiomba benki yake kuifungia lakini akajua
kwamba kadi yake ilikuwa tayari imetumika katika duka la mahali hapo, ambapo
watu wawili ambao inaonekana walikuwa hawana makazi walikuwa wameitumia kununua
kadi ya mwanzo ya ushindi.
"Walifurahi sana hivi kwamba walisahau
sigara na mali zao na wakatoka kama watu wazimu," wakili wa Jean-David
Pierre Debuisson alisema.
Alisema Jean-David amewasilisha malalamiko
ya polisi kuhusu wizi huo, lakini yuko tayari kuyaondoa iwapo wezi hao
watajitokeza ili wagawane fedha hizo.
"Ni hadithi ya ajabu, lakini yote ni
kweli," aliongeza.
Wakili huyo aliwasilisha rufaa ya kitaifa
siku ya Alhamisi, akiwataka wezi hao kuwasiliana na afisi yake ili kufanya
makubaliano.
"Bila wao, hakuna ambaye
angeshinda," aliambia shirika la utangazaji la Ufaransa-2.
La Francaise des Jeux (FDJ), mwendeshaji wa
bahati nasibu ya serikali, alisema bado hakuna mtu ambaye amewasilisha tikiti
ya kudai zawadi hiyo.
Bw Debuisson alisema waendesha mashitaka
wanaweza kujaribu kunyakua ushindi huo, kwa kuzingatia faida zilizopatikana
kinyume cha sheria, na akaonya kwamba tikiti itaisha.
"Wakati unafanya kazi dhidi
yetu," alisema.
"Huna hatari yoyote ... tutashiriki
nawe," alisema. "Na ungekuwa na uwezo wa kubadilisha maisha
yako."