
MSANII mwenye utata, Chris Embarambamba kwa mara nyingine amekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutoa wimbo kumuomboleza aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati.
Embarambamba alichapisha wimbo huo kwenye YouTube Jumamosi
Februari 22, siku moja tu baada ya familia kuthibitisha kifo cha afisa huyo wa
IEBC.
Katika wimbo wake, Embarambamba alimuomboleza Chebukati kama
aliyekuwa chanzo cha marais Uhuru Kenyatta na William Ruto kuongoza Kenya.
“Nitoboe siri, haki
wallahi Chebukati amelala, amekufa. Ndiye alifanya Uhuru [Kenyatta] akaongoza,
mtoto wa Kenyatta, Uhuru akaongoza… akasimama imara, Ruto akaongoza, Amen,” Embarambamba aliimba kwa
sehemu.
Aidha, katika vesi ya Pili, mwanamuziki huyo mwenye vimbwanga
alisimulia matukio yaliyokumba uongozi wa Chebukati katika tume huru ya
uchaguzi na mipaka IEBC, kutoka kwa kupigwa vita na baadhi ya makamishna wake
hadi wanasiasa.
Akizua utani katika maombolezo yake, Embarambamba alihoji
Chebukati aliiacha wapi familia yake lakini pia namba fiche ya M-Pesa yake.
“Chebukati umeacha wapi
familia yako… umeacha wapi PIN yako ya M-Pesa… Chebukati ulipitia mateso na
shida nyingi, mara kupigwa IEBC…” Embarambamba aliimba huku akimtuma
kuwapa salamu viongozi wengine wa Kenya waliotangulia mbele za haki.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa IEBC alifariki mwishoni mwa juma
lililopita wakati akitibiwa kwenye hospitali moja jijini Nairobi akiwa na umri
wa miaka 63.
Kifo chake kiliwagusa wengi, baadhi ya viongozi wa serikali
ya Kenya Kwanza wakitoa wito kwa serikali kumpa buriani ya kishujaa katika
mazishi ya kitaifa.
Kauli hizo ziliongozwa na mbunge wa Gatundu Kusini, Gabriel
Kagombe ambaye alimtaja Chebukati kama mtu aliyekuwa mwenye misimamo yake
asiyeweza tetereka licha ya shinikizo kubwa kutoka kwa pande hasimu kisiasa.
Alisema kwamba Chebukati alisimama imara kuhakikisha taifa
halikutumbukia katika dimbwi la machafuko ya baada ya uchaguzi katika uchaguzi
mkuu wa Agosti 2022, hivyo kudai haja kubwa ya yeye kupewa buriani ya hadhi ya
kitaifa.
“Mimi nasema kwamba
Chebukati ni shujaa ambaye anastahili kupatiwa heshima yake na mimi najua hata
nchi hii na serikali itampa mazishi ama buriani ya kufaa,” Kagombe alijieleza.