
KAMPUNI mama ya Facebook, Meta imetangaza kuanza kutekeleza kanuni ya kufuta kabisa video za moja kwa moja kwenye jukwaa hilo kila baada ya siku 30.
Katika chapisho kwenye tovuti rasmi ya Meta, kampuni hiyo
ilisema kwamba sasa watumizi wa Facebook wanaofanya video za moja kwa moja
watakuwa wanazipoteza kabisa pindi zinapomaliza siku 30.
Kanuni hiyo ilianza kutekelezwa Februari 19, ambapo Facebook
ilisema itakuwa inawatumia wamiliki wa video barua pepe kuwajulisha kuwa video
zao zinakaribia kumaliza siku 30, hivyo kufgutwa kabisa.
“Kuanzia tarehe 19
Februari, video za moja kwa moja zinaweza kuchezwa tena, kupakuliwa au
kushirikiwa kutoka kwa Kurasa za Facebook au wasifu kwa siku 30, na baada ya hapo
zitaondolewa kiotomatiki kwenye Facebook,” walitoa sasisho.
Hata hivyo, walisema kuwa barua pepe itampa mmiliki wa video
nafasi ya kukata rufaa ya kuongezewa siku zaidi kabla ya video zake kufutwa.
“Video za moja kwa moja ambazo zimehifadhiwa
zaidi ya siku 30 kwa sasa zitaondolewa kwenye Facebook. Kabla ya kumbukumbu
zako za moja kwa moja za video kufutwa, utaarifiwa kwa barua pepe na katika
programu, na kuanzia hapo utakuwa na siku 90 za kupakua au kuhamisha maudhui
yako.”
Meta ilisema kwamba itakuwa inakubalia rufaa ya hadi miezi 6
na baada ya hapo utazipoteza video zako zote za moja kwa moja kama hutakuwa
umezihifadhi kwa kuzipakua.
“Iwapo unahitaji muda wa
ziada ili kupakua video zako za awali za moja kwa moja, tunatoa chaguo la
kuahirisha ufutaji kwa miezi sita ya ziada. Baada ya kipindi hicho, ikiwa
hutafanya chaguo, video zako za awali za moja kwa moja zitaondolewa na
hazitapatikana tena.”
Facebook walitetea hatua hiyo wakisema kwamba ni njia moja ya
kuboresha jinsi watumizi wanaburudika na mitandao huo kuambatana na video za
usasa zaidi.
“Mabadiliko haya
yataoanisha sera zetu za uhifadhi na viwango vya sekta na kusaidia kuhakikisha
kuwa tunatoa hali ya utumiaji iliyosasishwa ya video za moja kwa moja kwa kila
mtu kwenye Facebook.”
Facebook walitangaza kuanzisha njia zingine zitakazowawezesha
watu kupakua video zao kwa wepesi zaidi katika siku za hivi karibuni.
“Mchakato wa kufuta
utafanyika kwa mawimbi katika miezi ijayo, na tunatoa zana mpya kwa watu
kupakua video zao za awali za moja kwa moja kabla hazijafutwa hatua kwa hatua.”