
MCHUNGAJI Robert Burale ameshangaza sehemu ya wafuasi wake kwenye mitandao ya kijamii baada ya kukata uteuzi wake kuwania tuzo ya ‘Most Inspirational Man of God 2025’.
Burale alikuwa ameteuliwa kuwania tuzo hiyo na wababe wa
injili kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika akiwemo Pastor T Mwangi lakini
akaomba wafuasi wake kutofanya uthubutu wa kumpigia kura.
Kwa mujibu wake, ni fahari kubwa kutambuliwa Afrika na
kuwekwa kwenye safu ya wanaostahili kuwania na kushinda lakini hahisi kama wito
wake kueneza injili unafaa kuwekwa kwenye mizani ya kupigiwa kura.
“Kwa jinsi ninavyothamini
uteuzi huo, nawaomba wafuasi wangu kwa unyenyekevu wasinipigie kura katika
kitengo hiki kwani siamini wito wa Mungu juu ya maisha yangu unapaswa kupigiwa
kura,” Burale alisema.
Mtumishi wa Mungu alishukuru waandalizi wa tuzo hizo kwa
kumteua lakini akisema hayuko tayari kushiriki katika kupigiwa kura, huku
akifichua kwamba tayari alikuwa amewasiliana naye kuwaeleza kwamba amejiondoa
rasmi hata kabla ya kura kupigwa.
“Kwa waandaaji asante kwa
ishara lakini ninaondoa jina langu kwa unyenyekevu. MUNGU AWABARIKI. Ninahubiri
tu kwa Neema ya Mungu ... kwa neema.”
“Nimewasiliana na
waandaji rasmi lakini nimeweka hili hapa kwa sababu wafuasi wangu wengi
wamenitumia ujumbe wakinihakikishia kura yao ...Kwa watu wote ninaowatia moyo
huko nje Mungu apate utukufu,” Burale aliongoza.