
GAVANA wa zamani wa Nairobi, Mike Sonko amekanusha uvumi kwamba amesafiri hadi nchini Vietnam kujadili uwezekano wa kuachiliwa kwa Mkenya Margaret Nduta dhidi ya hukumu ya kunyongwa.
Sonko alizungumza kupitia video ambayo alichapisha kwenye
kurasa zake mitandaoni akikanusha uvumi huo na kikariri kwamba bado yuko Kenya.
Uvumi wa Sonko kuenda nchini Vietnam ulizuka TikTok baada ya
yeye kuchapisha picha akiwa na raia kutoka bara la Asia, jambo lililowafanya
watu kudhani yuko Vietnam.
Hata hivyo, alisema kwamba watu hao, japo wanafanana na raia
wa Vietnam lakini ni wananchi wa Uchina ambao walimtembelea kwa mazungumzo ya
ushirikiano wa kibiashara.
“Nimeona mtu kule TikTok
akisema kwamba eti Sonko ametua nchini Vietnam kujadili kuachiliwa kwa Margaret
Nduta, Mkenya aliyetarajiwa kunyongwa usiku wa jana. Atafanikiwa? Kila la heri,” chapisho hilo kwenye
TikTok lilisomeka.
Sonko alicheka akisema kuwa huo ni mzaha uliotanuliwa nje ya
mipaka, akisema kwamba yeye dawa ambazo anajihusisha nazo katika nyumba yake ni
za kuzuia hatari za kiafya tu.
“Hii ni ile picha ya jana
na hawa ni wawekezaji kutoka Uchina na sasa watu wanasema eti hapa ni Vietnam. Lakini
hapa ni humu ndani ya nyumba yangu,” Sonko alieleza huku akifananisha
mandhari ya picha hiyo na madhari sawia ya ndani ya nyumba yake walikopigia
picha husika.
Mfanyibiashara huyo alimaliza kwa kutoa wito kwa serikali
kufanya juhudi zote kuzuia hukumu ya Nduta kunyongwa na ikiwezekana kurejeshwa
humu nchini.
Sonko alisema kwamba huenda msichana huyo alihadaiwa kubeba
mzigo wa mtu ambaye baadae ulikuja kugundulika kuwa na chembechembe za dawa
haramu nchini Vietnam, akitaka wahusika halisi kutafutwa.
“Hii kesi ya Margaret ni
ndogo sana, inasemekana alibebea mtu kwa jina John dawa. DCI hebu tusaidie huyu
msichana. Na njia pekee ya kumsaidia ni kutafuta mwenye alimsindikiza hadi
uwanja wa ndege – pengine ni huyo John.”
“Tuangalie deta za namba
ya simu ya mamake, alitoka Kenya lini, na kwa ile deta tutapata mwenye alimtuma
Margaret na dawa, huyo ndio anafaa ashikwe apelekwe anyongwe, Margaret
aachiliwe huru,” Sonko alieleza.
Nduta aliratibiwa kunyongwa usiku wa Jumatatu nchini Vietnam
baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya.
Hata hivyo, serikali ya Kenya kupitia wizara ya masuala ya
nje ilizungumza na Vietnam ambapo PS Korir Song’Oei aliwasiliana na mwenzako na
kuahidiwa muda zaidi kushughulikia kesi hiyo ngumu.