
MBUNGE wa Embakasi Mashariki, Babu Owino amekuwa wa hivi punde kutoa wito wa kipekee kwa rais William Ruto kuwasiliana na serikali ya Vietnam ili kuzuia kunyongwa kwa Mkenya Margaret Nduta.
Kupitia kurasa zake kwenye mitandao ya
kijamii, Owino alimrai rais Ruto kuwasiliana na mwenzake wa Vietnam ili kuzuia
kunyongwa kwa Mkenya huyo kunakotarajia kufanyika usiku wa Jumapili, Machi 16.
Margaret Nduta anasubiriwa hukumu yake ya
kunyongwa na serikali ya Vietnam baada ya kukutwa na dawa za kulevya katika
uwanja wa ndege.
Akimtetea, Owino alidai kwamba Nduta
hakutekeleza uhalifu wowote, bali yeye ni mwathirika wa matukio aliyejipata
katika sehemu mbaya wakati mbaya.
“Napenda kuchukua fursa hii kumuomba
na kumrai Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Ruto, amsaidie bibi huyu aitwaye
Margaret Nduta anayedaiwa kunyongwa kesho huko Vietnam, huyu bibi hakufanya
kosa lolote, alikuwa mahali pasipostahili kwa wakati mbaya, alitumika
kusafirisha dawa za kulevya,” alisema Babu.
Alipendekeza zaidi kwamba ikiwa mazungumzo
yatahitajika, Kenya inaweza hata kubadilishana afisa wa serikali fisadi kwa
uhuru wake.
"Hatufai kumpoteza Mkenya, Bw. Rais.
Unahitaji kuchukua hatua kwa haraka. Msaidie Margaret Nduta. Asinyongwe.
Ninajua kwamba unaweza kuchukua simu yako na kuipigia serikali ya Vietnam. Sisi
kama Wakenya tunahitaji kuungana nyuma ya bibi huyu. Hata ikimaanisha
kubadilishana naye mmoja wa Mawaziri fisadi, tufanye lolote tuwezalo kuokoa
maisha ya Margaret."
Huku muda ukizidi kuyoyoma, sasa
inasubiriwa kuonekana ni hatua gani ambayo itachukuliwa kuhakikisha hukumu hiyo
ya Nduta kunyongwa inahairishwa ili kutoa muda wa majadiliano zaidi.