
MCHEKESAHI na muigizaji, Eunice Mammito ametaka jumbe za kumhongera kwa kupata mtoto kutumwa kwake kwa njia ya miamala ya pesa.
Mama huyo mpya mjini alichapisha picha akiwa amempakata
mwanawe mchanga na kusema kwamba angependa wale wanaompa hongera kwa kuwa mama
kufanya hivyo kupitia jumbe za M-Pesa pekee.
Mammito alichapisha nambari ya till kwa ajili ya kufanikisha
miamala hiyo, akiashiria kwamba jumbe tupu za kumhongera hazina athari kwake na
ndio maana angependa kuhisi hongera za dhati kupitia kupokea pesa.
“Jumbe za hongera zikuje
kwa njia ya M-Pesa,” Mammito aliandika huku akifuatisha na nambari ya
Till.
Takwa hili linajiri saa chache tu baada ya mrembo huyo
kufichua kuwa yeye ni mama mpya, japo hakuweka wazi jinsi ya mwanawe.
Mammito alifichua kuwa mjamzito mwaka jana wakati wa Maandamano ya vijana wa Gen Z akisema kwamba alihisi ni wakati mwafaka kwake.
Akizugumza kwa mara ya kwanza kuhusu ujauzito wake Desemba
mwaka jana, Mammito alidinda kufichua mhusika, lakini akasema kwamba mimba yake
hakununua ila asingependa kufichua utambulisho wa mhusika.
“Hii mimba yangu sijanunua, ni ya mtu tu; ni kijana tu wa
watu na ni mtoto wa mtu Fulani,” Mammito alieleza.
Kuhusu ni kwa nini hayuko tayari
kumtambulisha mhusika huyo kwa mashabiki wake mtandaoni, Mammito alisema kuwa
anafanya hivyo ili kumkinga yeye na pia mwanawe kutoka kwa hukumu hasi za watu
wa mitandaoni.
‘Lazima wafichwe hii Nairobi. Huwezi jua.
Useme ndio huyu waseme ooh hakai vizuri na wengine wamchukue na mimi sasa hivi
nina umri wa miaka 31, sitaki kuanza kuuliza mtu eti rangi uipendayo ni gani,
katika huu umri nimeshakua sasa, unaelewa,” Mammito alifafanua.
Katika mahojiano hayo na runinga ya TV47, Mammito pia
alikanusha tetesi kwamba mhusika alikuwa mpenzi wake wa zamani, Eddie Butita na
kusema baba wa mwanawe mtarajiwa alikuwa mtu asiye maarufu mitandaoni.
“Mimi na Butita ni maneno ya kale, ni muda mrefu uliopita
kama miaka 4 iliyopita. Kwa huyu, ni mtu ambaye si maarufu mitandaoni. Na
nafikiri mtu wa aina hiyo ndiye nilikuwa nataka, mwenye anajishughulisha na
mambo tofauti kabisa na tasnia yetu ya mitandaoni.”