
YOUTUBER Diana Marua amemshauri mwanawe wa kiasili Morgan Bahati kutokuwa na hulka ya kuchumbiana na wapenzi wengi kwa wakati mmoja kama ambavyo yeye alifanya katika maisha yake ya ujana.
Kupitia kipindi chake cha maswali na majibu na Morgan kwenye
chaneli yake ya YouTube, Diana Marua alimtaka Morgan kumuuliza swali lolote na
angeweza kumpa jibu kwa ufasaha.
Morgan alitaka kujua ni jambo lipi baya ambalo Diana alifanya
katika maisha yake ya ujana na ambalo asingependa yeye [Morgan] kulifanya.
Bila woga, Diana alisimulia kwa majuto jinsi alijiingiza
katika harakati za kuingia katika mahusiano ya mapenzi na wanaume kadhaa kwa
wakati mmoja, akisema ni jambo ambalo asingependa limtokee Morgan.
“Kuna vitu vingi ambavyo
nilivifanya kama tineja na ambavyo sijivunii kusema ukweli. Jambo la kwanza
katika umri wangu wa ujana nilichumbiana na watu wengi. Kwa ufupi ni kwamba
sikuwa muaminifu kwa mpenzi mmoja,” Diana alifungua jungu kuu la siri.
Kulingana naye, hulka hii ya kuwa na wapenzi wengi kwa mpigo
ili mpotezea bahati yake ya kumpata hata yule ambaye alifikiria angemfaa katika
maisha yake kimapenzi.
“Hiyo ilinigharimu sana
maana mwisho wa siku walikuja kugundua na ilizua tafrani sana. Na hata kwa
wakati mmoja waliungana dhidi yangu na unajua siku moja walikuja wote kwa
pamoja.”
“Na katika mfarakano huo
niliishia kumpoteza hata yule ambaye nilikuwa nafikiria alikuwa wangu wa
kufaana naye. Na mwisho wa siku nilipoteza wote. Nilikuwa msichana mbaya. Na hicho
ndicho kitu kimoja ambacho nisingependa wewe ufanye,” Diana alimaliza kwa
ushauri.
Mama huyo wa watoto 3 alimshauri Morgan kujifunza kusema ‘hapana’
kwa vitu ambavyo havipendi ama vile ambavyo haviendani na falsafa yake ya
maisha.