Mwanawe sosholaiti wa Uganda Zari Hassan, Raphael Tlale
amefunguka kuhusu maisha yake ya uchumba na aina ya wanawake anaowapendelea.
Katika mahojiano na Mpasho, Raphael ambaye ni mtoto wa pili wa Zari aliweka wazi kuwa anapenda wanawake, na kukanusha madai ya awali kuwa yeye ni shoga.
Raphael alielezea kuhusu matamshi ya utata
ambayo alitoa miaka kadhaa iliyopita alipoingia kwenye live ya Instagram na
kudai kuwa shoga.
"Kwangu mimi, najua sio shoga. Nilisema, hata kama kila mtu anasema hivyo, najua maisha yangu kwa hivyo hakuna mtu anayeweza kunifanya nibadilishe jinsi ninavyofikiri na jinsi ninavyohisi,” Raphael alisema huku akifichua kuwa alitoa matamshi yake ili kuwahimiza vijana wapenzi wa jinsia moja kuwa na ujasiri kuwaambia wazazi wao kuhusu hilo.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 20 alikwepa kuthibitisha kama anachumbia na mtu yeyote lakini akakiri kwamba kuna msichana anayempenda.
“Kuna msichana ninayempenda. Ndiyo. Lakini sichumbii,” alisema.
“Sijamwambia kuwa nampenda. Sijui ni lini nitamwambia, kwa kweli sina haraka. Ninangojea tu wakati unaofaa kisha nichukue hatua sahihi. Sina haraka sana kutafuta msichana sasa hivi. Ninajaribu kujijenga kwanza. Wasichana daima watakuwa hapa. Wakati nitakapojifanya kuwa mwanamume, basi naweza kufikiria kuongeza mtu katika maisha yangu,” aliongeza.
Raphael alipoulizwa sifa ambazo yeye hutazama kwa mwanamke, alisema kuwa anapenda wanawake wazuri, wapole, waaminifu na wanaoweza kuwasiliana vizuri.
Pia alifichua kuwa anapendelea kuchumbiana na wanawake ambao ni wakubwa kuliko yeye kwani ana mapendeleo tofauti na wenzake.
"Napenda wanawake wakubwa. Ninahisi kiwango changu cha ukomavu ni tofauti. Njia ninayofikiria ni tofauti. Ikiwa ninazungumza na mtu, napenda mambo yawe mazito sana. Watu wa rika langu wanapenda kujifurahisha, kuchunguza na kutochukulia mambo kwa uzito. Nahisi mtu mkubwa ataelewa,” alisema.
Raphael pia alifichua kuwa mamake Zari Hassan mara nyingi humpa ushauri wa kimahusiano na kumwonya kuhusu wanawake wa kuchumbiana na wale wa kuepuka.