
Mcheza santuri mashuhuri wa Kenya Samuel Muraya almaarufu DJ Mo amechukua hatua kubwa katika ndoa yake ya kumvisha pete ya uchumba mpenzi wake wa muda mrefu Linet Munyali almaarufu Size 8, hatua ambayo imewashangaza wengi.
Wawili hao mnamo Agosti mwaka jana walitangaza kusambaratika kwa ndoa yao ya miaka kumi na moja, na hawajawahi kuthibitisha kurudiana tangu wakati huo.
Siku ya Ijumaa hata hivyo, ulimwengu ulipokuwa ukiendelea kusherehekea siku ya wapendanao, wazazi hao wa watoto wawili walichapisha video nzuri inayoonyesha wakati muhimu katika maisha yao.
Katika video hiyo, wawili hao walionekana katika mazingira mazuri ya kimahaba ambapo DJ Mo alimuuliza mama wa watoto wake wawili iwapo atakuwa mke wake. Size 8 alionekana kukubaliana na ombi hilo na walionekana wakibusiana kwa furaha nyusoni mwao.
"Tunamshukuru Mungu kwa kubariki ndoa yetu na kuweka upendo wetu kuwa imara katika kila changamoto," DJ Mo aliandika chini ya video aliyoweka kwenye Facebook.
“Haijalishi vizuizi vinavyotujia, Bwana alitupa neema ya kushinda na kwa hivyo tuliweza kuchagua kupendana. Hili ndilo tendo la Bwana... Kwa hakika kile ambacho Mungu hawezi kufanya, hakipo. Sifa na Utukufu zote zimwendee Mungu Baba yetu kwa njia ya Yesu Kristo. Upendo haushindwi kamwe” 1 Wakorintho 13:8 ❤️,” aliongeza.
Hatua hii imekuja kwa mshangao kwani wengi walidhani kuwa wasanii hao wawili bado wametengana, kwani walitangaza kuachana mwaka jana.
Mwezi Agosti mwaka jana, Size 8 ambaye ni mhubiri na mwimbaji wa nyimbo za injili, alitangaza kuvunjika kwa ndoa yake ya miaka kumi na moja.
Katika taarifa fupi tarehe mosi mwezi huo, mama huyo wa watoto wawili alitangaza kwamba anaanza safari ya kuwa bila mume.
Size 8 amekuwa kwenye ndoa na mcheza santuri DJ Mo kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita na wana watoto wawili pamoja.
"Wakati mwingine ndoa hufanya kazi kwa neema ya Mungu, na wakati mwingine haifanyi kazi, lakini yote kwa yote Mungu bado yuko kwenye kiti cha enzi," Size 8 alisema kupitia Instagram.
Aliongeza, "Nimeolewa kwa miaka 11 na sasa ninaanza safari ya kuwa mseja. Lakini Mungu bado yuko kwenye kiti cha enzi, nakuabudu wewe Yaweh!"
Hata hivyo, mwanamuziki huyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu hali ya ndoa yake au sababu iliyosababisha yeye kutengana na mzazi mwenzake.