
MJASIRIAMALI na msanii Akothee amejitokeza kimasomaso kutetea baba wa wanawe akisema kwamba wako na kila haki ya kusherehekea mafanikio ya wanao.
Akothee alikuwa anamtetea baba wa wanawe, Jared Okello
aliyeonekana kusutwa baada ya kuonekana kwenye hafla ya binti yake na Akothee
ambaye alikuwa anatambulisha mpenzi wake kwa wazazi wake.
Akothee alimtetea kutoka kwa wale waliokuwa wakimshambulia, akisema
kwamba wazazi wenzake wote wamekaribishwa muda wowote kusherehekea mafanikio ya
watoto wao.
Kwa mujibu wa Akothee, wazazi wenzake wanakaribishwa
kusherehekea naye mafanikio ya wanao bila kujali kama walimsaidia katika malezi
au la.
“Baba watoto wangu wote
wanakaribishwa kusherekea mafanikio ya watoto wetu iwe nilifanya peke yangu au tulishirikiana
nao. Siwezi kujipa mimba mwenyewe. Baba watoto wangu wana nafasi kubwa katika
maisha yangu. Walinibadilisha kutoka kwa
msichana hadi kuitwa "mummy", imeishia hapo,” Akothee alisema.
Alimsifia Okello kwa kuweka msingi bora kwa wanawe licha ya
penzi lao kuvunjika baadae na kusema kwamba kwa hilo, hawezi simama kando
akiona mwanamume huyo akikosewa heshima kwa njia yoyote ile.
“Sitasimama na kutazama
mtu yeyote akimtupia dongo baba wa watoto wangu. Jared Okello Otieno ndiye baba
mzazi wa watoto wangu wanne, na hakuna kitakachobadilisha hilo.”
“Mwanamume huyu aliweka
msingi wa nidhamu katika familia yetu na alikuwa baba wa mfano kabla mambo
hayajabadilika na muungano wetu haujafikia kikomo. Lakini hiyo haimaanishi
kwamba yeye ni mtu mbaya au kwamba hatakiwi kusherehekea mafanikio ya watoto
wake—hata hivyo! Tunabaki kuwa familia, iliyounganishwa sana, licha ya kwenda
njia zetu tofauti. Ninatekeleza jukumu langu kama mama yao, huku nikiheshimu
pia uwepo wa mtu ambaye ninawajibika sawa kwake,” Akothee aliongeza.
Wikendi iliyopita, Akothee alijumuika na wanafamilia wake
kuhudhuria hafla ya kuhalalishwa kwa uchumba wa bintiye, Fancy Makadia nchini
Ufaransa.
Fancy Makadia ambaye jina halisi ni Prudence na mpenzi wake
Fairouz walihalalisha uhusiano wao mnano Machi 22 nchini Ufaransa.
Akothee alikanusha kwamba hafla hiyo ilikuwa ya harusi
akithibitisha kwamba harusi yenyewe itafuata baadae, huku akionyesha furaha ya
subira yake kwa siku hiyo kuu.