
Mchekeshaji mkongwe kutoka Tanzania, Rashid Mwinshehe maarufu kama Kigwendu, amefunguka kuhusu changamoto kubwa anayopitia kwa sasa, hasa katika suala la usafiri..
Msanii huyo maarufu ameeleza kuwa kutokuwa na gari kumemuweka katika hali ngumu, kiasi cha kuathiri kazi zake za sanaa na maisha yake kwa ujumla.
Katika mahojiano ya hivi majuzi, Kigwendu alisema kuwa analazimika kutumia daladala kama njia yake ya usafiri wa kila siku, hali inayomsababishia usumbufu mkubwa.
Kutokana na umaarufu wake, mara nyingi anajikuta akichekwa na abiria wenzake, jambo linalomdhalilisha na kumfanya ajisikie vibaya.
“Kwasasa siwezi kufanya kazi zangu kwa ufanisi wala kusaidia familia yangu kwa sababu sina usafiri. Nikikosa usafiri wa uhakika, inakuwa vigumu kuzunguka mjini kutafuta riziki. Kuna siku ambapo nikipata nafasi ya kufanya kazi vizuri, naweza kupata hadi shilingi laki nane kwa siku, lakini bila usafiri, mambo hayaendi kama inavyotakiwa,” alisema Kigwendu.
Akiendelea kufafanua, alieleza kuwa matatizo yake ya kifedha yalianza alipoweka mguu kwenye siasa.
Alisema kuwa alipopata madeni makubwa, ilibidi auze magari yake yote ili kujaribu kujinasua kiuchumi, lakini bado hali haijawa nzuri.
“Kwasasa naishi mbali, Nzasa, na kila ninapotaka kwenda kwenye shughuli zangu, napata changamoto kubwa ya usafiri. Gharama za nauli ni kubwa na mara nyingi inabidi nitumie pikipiki au daladala, jambo ambalo linanifanya nichekwe na mashabiki wangu barabarani,” alisema Kigwendu.
Kwa sababu hiyo, ameomba msanii mkubwa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, amsaidie kumpatia gari hata dogo ili aweze kurahisisha shughuli zake za kila siku.
“Naomba kama inawezekana, Mwenyezi Mungu amjalie Diamond moyo wa ukarimu anisaidie hata kwa gari dogo, hata IST, ili nipungukiwe na changamoto ya usafiri. Kwa sasa ninalazimika kutumia pikipiki na daladala, ambapo mara nyingi mashabiki wangu wananiangalia kwa mshangao na wengine hufanya mzaha nami barabarani. Hii inanifanya nijisikie vibaya sana,” alisema Kigwendu kwa uchungu.
Kigwendu anasema ukosefu wa usafiri umemzuia hata kuwaona ndugu zake walioko mbali, hali inayomfanya ajihisi mpweke. Anasisitiza kuwa gari litamsaidia kujipatia kipato zaidi na kurejesha heshima yake mitaani.
Kwa muda mrefu, Kigwendu amekuwa mmoja wa wachekeshaji maarufu nchini Tanzania, akijulikana kwa vichekesho vyake vya kipekee ambavyo vimewafanya mashabiki wake kumpenda. Hata hivyo, changamoto za kimaisha zimeathiri ustawi wake katika tasnia ya burudani, hali inayomfanya aombe msaada ili aweze kurejea katika hali nzuri na kuendelea kuburudisha mashabiki wake.