
VITA vya maneno kati ya mbunge wa Kapseret Oscar Sudi na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna imeendelea kuchukua mikondo tofauti baada ya mbunge huyo kuruasha kombora katika kambi ya Sifuna.
Sifuna awali alikuwa amemkashifu Oscar Sudi akidai kwamba
rais William Ruto anajishusha hadhi kuwa karibu na mbunge huyo.
Kwa mujibu wa Sifuna, rais Ruto anashusha hadhi yake kwa
kutembea na Sudi ambaye alimtaja kama mtu mwenye ujuzi wa darasa la pili tu.
“Ruto alituambia kwamba
ana PhD, mimi sijawahi ona mtu wa PhD anayetembea na mtu aliyeachia shule
darasa la pili. Inawezekana aje wewe una PhD na unatembea na Sudi. Inawezekana aje
hiyo kuwa ukweli,” Sifuna alisema katika mahojiano na runinga ya Citizen
TV.
Tamko hili lilionekana kumuuma Sudi ambaye kupitia ukurasa
wake wa X aliachia video akimzomea Sifuna.
Mbunge huyo wa Kapseret alisema kwamba Sifuna anaweza kuwa na
elimu ya kiwango cha juu lakini katika ujuzi hafikii hata robo ya ujuzi wake
yeye.
“Sifuna unaweza
jilinganisha na mimi? Unajua IQ yangu na yako hazilingani hata kwa robo. Tafuta
mtu mwingine ambaye unaweza jilinganisha naye au mwenye utalinganisha na Ruto,” Sudi alimwambia.
“Mimi niko katika kiwango changu na sio kwamba ninaringa au nini lakini unaweza ulizia kuhusu historia yangu. Huna hata robo ya ujuzi wangu. Kwa hivyo usikuwe mpuuzi kuongea kama mtoto,” Sudi aliongeza.
Sudi alisema kwamba Sifuna amekuwa na hulka ya kushambulia
kila mtu akidhani ni haki yake, lakini kwake amefika kwenye mwamba.
“Sio kuhusu shule, la
maana ni kuwa na ujuzi. Sio kuhusu PhD, ni kuhusu hesabu. Mradi tu unaweza ona,
unazungumza, unaweza ona na hata kunusa… wewe sidhani uko na hizo zote. Wewe ni
mtu tu bure, mpuuzi,” Sudi alimaliza.