
Licha ya changamoto za kiafya, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alipata muda wa kuomba katika kanisa dogo ndani ya hospitali na kushiriki katika baadhi ya shughuli za kikazi.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Habari ya Vatican, “Hali ya Baba Mtakatifu ni imara ndani ya hali ambayo bado ni changamoto kwa ujumla. Utabiri wa afya yake bado unachunguzwa kwa makini.”
Papa anaendelea kupokea matibabu ya kifua, ikiwa ni pamoja na tiba ya kusaidia kupumua, ambapo anatumia mashine ya kupumulia kwa njia isiyo ya uvamizi usiku na oksijeni yenye mtiririko wa juu mchana kupitia mrija wa pua.
Kutokana na hali yake kutokuwa na mabadiliko makubwa, Vatican ilieleza kuwa taarifa kamili kuhusu afya yake itatolewa Jumamosi.
“Kama ilivyotangazwa awali, hakuna taarifa mpya ya kiafya itakayotolewa jioni hii kutokana na utulivu wa hali yake. Hata hivyo, taarifa mpya itatolewa kesho, Jumamosi, Machi 8,” Vatican ilisema.
Mapema Ijumaa, ripoti zilisema kuwa Papa Francis alipata usingizi mzuri na aliamka muda mfupi baada ya saa mbili asubuhi kwa saa za Rome.
Maombi ya Rozari kwa ajili ya Papa yaliendelea kufanyika Ijumaa usiku katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, yakiendeshwa na Kardinali Lazzaro Heung-sik You, Mkuu wa Idara ya Wakleri Vatican.
Waumini wa Kanisa Katoliki kote ulimwenguni wanaendelea kumuombea Baba Mtakatifu apone haraka na kurejea katika shughuli zake za kichungaji.