
Licha ya kuwa hospitalini akipokea matibabu, Kiongozi wa
Kanisa Katoliki, Papa Francis, alishiriki Ibada ya Jumatano ya Majivu katika
makazi yake binafsi kwenye Hospitali ya Gemelli, Roma.
Taarifa ya Ofisi ya Habari ya Vatican siku ya Jumatano jioni ilieleza kuwa hali yake ya kiafya imebaki kuwa thabiti, ingawa bado anapokea oksijeni ya mtiririko wa juu na anatumia msaada wa upumuaji kwa njia zisizo vamizi wakati wa usiku.
"Baba Mtakatifu aliendelea kuwa thabiti leo, bila tukio lolote la upungufu wa kupumua," ilisomeka taarifa hiyo.
"Kama ilivyopangwa, alitumia oksijeni ya mtiririko wa juu, na usiku huu ataendelea na tiba ya upumuaji kwa njia zisizo vamizi."
Hata akiwa hospitalini, Papa Francis aliendelea na shughuli zake za kiroho na kikazi.
Katika ibada ya Majivu iliyofanyika asubuhi katika chumba chake cha makazi, alipakwa majivu kichwani mwake na mhudumu wa ibada, kisha akapokea Ekaristi, ilisema taarifa hiyo.
Mbali na ibada hiyo, alitumia sehemu ya siku kwenye kiti chake, akiongeza tiba ya kupumua na mazoezi ya mwili, huku akihusika katika shughuli mbalimbali za kazi.
Papa Francis pia alichukua muda kuwasiliana na Padre Gabriel Romanelli, kasisi wa Parokia ya Holy Family iliyoko Gaza.
"Katika kipindi cha asubuhi, Baba Mtakatifu alimuita Padre Romanelli wa Gaza," taarifa ya Vatican ilifafanua, hatua inayoonyesha mshikamano wake na waumini katika eneo hilo lenye changamoto.
Mchana, alichanganya kati ya kazi na mapumziko. Licha ya juhudi za kuimarisha afya yake, Vatican imeendelea kuwa na tahadhari kuhusu maendeleo yake ya kiafya.
"Kutokana na hali changamano ya kiafya, bado kuna
tahadhari kuhusu maendeleo ya matibabu," ilieleza taarifa hiyo.
Papa Francis, ambaye ana umri wa miaka 87, ameendelea kuonesha moyo wa kujitoa kwa waumini wake hata wakati wa changamoto za kiafya.
Ushiriki wake katika ibada hii muhimu ya Kikatoliki
unathibitisha dhamira yake ya kudumu katika huduma kwa Kanisa.