
GAVANA wa Kisii, Simba Arati ametoa ahadi ya shilingi laki moja kwa yeyote atakayemkatama na kumchoma mwizi wa mifugo katika mpaka wa Kisii na Narok.
Akizungumza Jumatatu katika eneo la mpakani mwa Bomachoge Borabu
na Trans Mara wakati wa mkutano wa kutafuta suluhu ya amani uliowakutanisha
wananchi na viongozi kutoka jamii za Abagusii na Maasai, Arati alisema kwamba
ni sharti suluhu dhidi ya wizi wa mifugo lipatikane na liwe la kudumu.
Gavana huyo alitoa ahadi kwa wananchi kumkamata mwizi wa
mifugo na kumteketeza katika eneo hilo la mpaka na pindi taarifa hizo
zitakapomfikia, atatoa kima cha shilingi 100k.
“Mkichoma mniambie gavana
tulichoma mwizi hapa Trans Mara, ama hapa Kisii, na huyo yuko hospitalini
anapona. Nitapeana shilingi elfu 100 kwa kuchoma mwizi. Hiyo biashara ndio
tumalize,” Arati alisema.
“Hata hao wezi wakiwa 10,
niko tayari kutoa shilingi milioni moja. Unajua wakati mwingine tunacheza na
moto sana. Mtoto anaangusha moto hapa na nyumba yote inashika moto. Hatutaki biashara
kama hiyo. Kuanzia sasa mimi niko tayari,” gavana huyo aliongeza.
Kiongozi huyo ambaye ni naibu wa chama cha ODM alisema kwamba hata gavana mwenzake wa Narok, Patrick Ole Ntuntu ameafiki na hilo, akisema kwamba wakati mwizi atachomwa atachangia hela kuwatunuku vijana.
‘Hata huyo ni mtu ako na
pesa, gavana usijali nikikufikia nikwambie kwamba nimefika milioni moja au
mbili tumechoma wezi 20, wewe utaniongeza milioni nyingine tukawape watu kwa
kazi nzuri. Kwa sababu hakuna haja ya kuzungushana namna hii, watoto wanafaa
kuwa shuleni, lakini eti kwa sababu ya vita watoto hawawezi enda kusoma. Kina mama
ambao wamepanda mboga pande hii hawawezi peleka mboga sokoni, hii upuzi lazima
iishe,” Arati alitema moto.
Vita baina ya jamii hizo mbili vimekuwa kwa takribani wiki
mbili sasa chanzo kikisemekana kuwa ni kuibwa kwa ng’ombe wawili.
Makumi ya vijana wamejeruhiwa huku takribani 3 wakiripotiwa
kufa kutokana na majeraha ya mishale na panga.
Jumatatu, waziri wa masuala ya ndani Kipchumba Murkomen
alitoa onyo kali kwa watu wanaotembea na silaha katika eneo hilo la mpakani
akisema kwamba vyombo vya dola vitaanza sakasaka za kuwakamata wote
watakaopatikana wakizurura na silaha.