
KINARA wa chama cha ODM Raila Odinga ameendelea kutetea muungano wa chama chake na kile cha UDA mwishoni mwa juma lililopita.
Akizungumza katika hafla Moja ya mazishi katika kaunti ya Kiambu Jumanne, Odinga alipuuzilia mbali tetesi kwamba yeye ndiye alimfuata rais Ruto na kuomba waungane.
Kwa mujibu wa Odinga, rais Ruto ndiye alimfuata na kumuomba kufanya kazi pamoja na Wala si yeye aliyemfuata rais.
“Watu wengi wanapiga kelele hapa na pale wakisema nilimfuata Ruto; kwamba Raila amemfuata Ruto na kutuacha. Sikumfuata Ruto, ni Ruto ndiye aliyenitafuta,” alisema Bw. Odinga.
Kiongozi huyo mkongwe katika siasa za upinzani nchini aidha alisisitiza kwamba kuungana kwake na Ruto hakujabadilisha misimamo yake kuhusu kutetea wananchi.
Alitolewa mfano maandamano ya mwaka 2023 ambapo yeye na wafuasi wake waliandamana kuishinikiza serikali kushukisha gharama ya maisha.
“Nafasi yangu kuhusu masuala ya kitaifa haijabadilika. Katika maisha yangu yote, nimekuwa nikisimama kwa ukombozi na ustawi wa wananchi. Mnajua kwamba mnamo 2023 tuliandamana kupinga gharama kubwa ya maisha. Wakenya walisema kuwa gharama ya maisha ilikuwa mzigo kwao,” aliongeza.
Katika hafla hiyo ya mazishi, Odinga alitupa dongo kwa serikali akikashifu kutofanya kazi kwa bima ya SHA.
"Nimemwambia Ruto kwamba SHA ina matatizo na inapaswa kurekebishwa. Ushuru unaowekewa Wakenya pia ni wa juu sana, hasa wa nyumba,” Raila alisema.
Akionekana kutetea kuungana kwa UDA na ODM, Raila alisisitiza kwamba ukosoaji kama wa kutofanya kazi kwa SHA hakuwezekana kama mtu Ako nje ya serikali.
“Mambo haya hayawezi kurekebishwa ukiwa nje, lazima uingie ndani na kuwaambia cha kufanya. Na lazima uweke watu mahali hapo kushughulikia matatizo hayo,” aliongeza Bw Odinga.