
KINARA wa chama cha ODM, Raila Odinga amesisitiza kwamba hakuna Mkenya yeyote ambaye alisaliti wakati aliamua kushikana na rais William Ruto mwishoni mwa juma lililopita.
Akizungumza katika hafla ya mazishi katika
Kijiji cha Nyaduong’, Wadi ya God Jope, Eneobunge la Suna Mashariki, Kaunti ya
Migori Jumapili, Odinga alisema kwamba kushikana kwa ODM na UDA ni kwa maslahi
ya wananchi wanaotaka maendeleo.
Alisisitiza kwamba yeye si msaliti kama
ambavyo sehemu ya Wakenya walihisi baada ya kutia Saini mkataba wa makubaliano
ya kufanya kazi Pamoja kati ya ODM na UDA.
“Msaliti ni nani? Hakuna mtu tumesaliti.
Sisi tuliandika mambo 10 muhimu zaidi, tukasema haya mambo yakirekebishwa tuko
tayari kufanya kazi sawa sawa,” Odinga
alisema.
Ni kauli ambayo ilisisitizwa na rais Ruto
ambaye alikuwa katika ibada ya kanisa kaunti ya Uasin Gishu, akisema kwamba
makubaliano ya oni ya kuhakikisha hakuna eneo la nchi ambalo litasalia nyuma
kimaendeleo.
“Hakuna jamii au eneo la Kenya ambalo
litasalia nyuma kimaendeleo,” Ruto alisema.
Hata hivyo, sehemu ya Wakenya wanaendelea
kuhisi kwamba Odinga hakufaa kuungana na rais Ruto na kutoridhishwa huku
kulishuhudiwa katika kaunti ya Kisii wakati wakaazi waliondoka kwa manung’uniko
mengi baada ya Odinga kuwasili.
Mashabiki wengi waliokuwa wakijumuika katika
uwanja wa Gusii kwa hafla ya uzinduzi wa jezi mpya za klabu ya Shabana FC
waliondoka kwa ghadhabu wakionesha kutoridhishwa kwao na hatua ya Odinga
kuungana na rais Ruto.
Mwishoni mwa juma lililopita, viongozi hao
wawili walitia Saini mkataba wa makubaliano ya kufanya kazi Pamoja huku wakisisitiza
jumla ya masuala 10 ambayo yatafanikishwa na ukuruba huu mpya.
Yafuatayo ni mambo hayo makuu ya mkataba wa
UDA-ODM:
1. Utekelezaji kamili wa ripoti ya Nadco
(Kamati ya Mazungumzo ya Kitaifa).
2. Ushirikishwaji katika mgao wa bajeti na
uteuzi wa umma
3. Kulinda na kuimarisha ugatuzi
4. Uwekezaji wa kiuchumi kwa vijana
5. Uongozi, uadilifu & mwisho wa kuonyesha
utajiri
6. Haki ya kukusanyika kwa amani, fidia ya
madai yote yanayosubiri ya waathiriwa wa haki
7. Ukaguzi wa deni la Taifa na jinsi
lilivyotumika
8. Kupambana na rushwa
9. Kukomesha ufujaji wa rasilimali za umma
10. Kulinda uhuru wa watu, kukomesha utekaji,
kuheshimu katiba na utawala wa sheria na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari.