
ALIYEKUWA gavana wa kaunti ya Meru, Askofu Kawira Mwangaza ametangaza kuwa ana jambo lake kuu kwa wafuasi wake usiku wa leo Machi 18.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mwangaza aliwataka wafuasi
wake kuwa ange kupokea tangazo lake ambalo aliweka wazi kwamba litakuwa ni
tangazo lenye dhumni kuu la kisiasa.
“Leo usiku kupitia kurasa
zangu za mitandao ya kijamii, nitakuwa natoa taarifa yenye madhumni ya kisiasa.
Tafadhali jiunge na sisi kutoka starehe ya sebule yako kuanzia saa mbili usiku,” Mwangaza alichapisha.
Hii ni mara ya kwanza kwa gavana huyo wa zamani kuvunja kimya
chake tangu kuapishwa kwa gavana mpya Jumatatu asubuhi.
Kuapishwa kwa gavana mpya – ambaye ni aliyekuwa naibu wa
Mwangaza, Isaac Mutuma, kulimaliza kivangaito cha kisiasa cha zaidi ya miaka
miwili ambacho kimekuwa kikishuhudiwa kati ya Kawira Mwangaza na bunge la
kaunti ya Meru.
Masaibu ya Mwangaza yalianza miezi 5 tu baada ya kuapishwa
kwake kama gavana baada ya kushinda kwa tikiti ya mgombea huru katika uchaguzi
wa 2022.
Wawakilishi wadi walimbandua lakini seneti ikabatilisha
uamuzi huo, lakini bunge la kaunti halikuridhika na lilirejesha hoja ya
kutokuwa na Imani naye bungeni mwaka jana na hatimaye kumbandua tena.
Safari hii, Mwangaza alitupwa chini ya lori na seneti, japo
uamuzi huo wa seneti ulipigwa breki na mahakama mnamo Agosti mwaka jana.
Uamuzi wa mahakama ulitolewa Ijumaa iliyopita ya Machi 14 na
jaji Bahati Mwamuye ambaye alisema Mwangaza alipewa muda stahiki wa kujitetea
kwenye seneti kinyume na pingamizi lake kwamba hakusikilizwa ipasavyo na
maseneta.
Jaji hivyo alidumisha uamuzi wa seneti, kumaanisha kwamba
Mwangaza alikuwa amebanduliwa ofisini rasmi na saa chache baadae, serikali
ilichapisha notisi kwenye gazeti rasmi la serikali kuhusu kuapishwa kwa Isaac
Mutuma.
Mutuma alikula kiapo Machi 17 katika hafla ambayo
ilihudhuriwa na viongozi wa zamani na wa sasa katika nyadhifa mbalimbali kwenye
kaunti hiyo.
Tetesi zinadai kwamba Mwangaza anatarajiwa kutangaza chama
chake cha kisiasa, saa chache tu baada ya kujiondoa kwenye chama tawala cha
UDA.