
Mahakama kuu imeidhinisha kuondolewa afisini kwa kwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza ikisema mchakato uliopelekea kuondolewa kwake ulifuata sheria.
Jaji Bahati Mwamuye siku ya Ijumaa alitupilia mbali ombi la Mwangaza akieleza kuwa mchakato wa kumfurusha ulifuata taratibu za kisheria.
"Ombi lililorekebishwa la Desemba 23, 2024, halijafikia kiwango cha kisheria kinachohitajika kwa mahakama hii kubatilisha uamuzi wa Seneti," jaji alitoa uamuzi huku akitupilia mbali ombi la Mwangaza.
"Ilani ya gazeti la serikali ya Agosti 20, 2024, iliyotolewa na Seneti ikiwasilisha uamuzi wa kumwondoa mlalamishi afisini kama gavana wa Meru, mashtaka yamethibitishwa," Jaji Mwamuye aliamua.
Gavana Mwangaza alikuwa amepinga kuondolewa kwake madarakani akiibua sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na madai ya ukiukwaji wa taratibu, kusikilizwa kwa haki na madai ya kutoshirikishwa ipasavyo kwa umma.
Bi Mwangaza alikuwa mmoja wa magavana saba wa kike waliochaguliwa baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 huku akijizolea kura 209,148 na kumwangusha aliyekuwa gavana Kiraitu Murungi na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi.
Jumla ya maseneta 26 walipiga kura kuunga mkono mashtaka matatu yaliyofikishwa dhidi ya Bi Mwangaza.
Lakini alikimbilia kortini siku iyo hiyo na Jaji Mwamuye akasimamisha utekelezaji wa azimio la Seneti, kumwondoa afisini.
Bunge la Seneti lilipinga agizo la kusitisha kuondolewa kwake likisema kwamba agizo hilo lilikuwa linaingilia mamlaka ya maseneta.
Seneti pia lilisema kwamba halikupewa fursa ya kusikilizwa kabla ya agizo hilo kutolewa. Maseneta walisema agizo hilo lilikuwa linakiuka kanuni za haki asilia, ambazo zinahitaji kwamba pande zote zina haki ya kusikilizwa kabla ya uamuzi wowote kutolewa.
Kawira hata hivyo anatarajiwa kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama kuu.