
NAIBU wa rais profesa Kithure Kindiki amesisitiza kwamba ziara ya rais William Ruto katika ukanda wa Mlima Kenya kuanzia wiki ijayo haitakuwa ya kisiasa.
Akizungumza katika kaunti ya Murang’a Alhamisi, Kindiki
aliweka wazi kwamba ziara hiyo ya wiki moja ya rais Ruto Mlimani itakuwa tu ya
kuzindua miradi iliyokamilika na mingine itakayoanza kutekelezwa.
Kulingana na Kindiki, Ruto atakuwa akizindua masoko
yaliyojengwa na serikali na kuyakabidhi kwa wafanyibiashara, ujenzi wa barabara
miongoni mwa miradi mingine.
“Wiki ijayo, Mungu
akipenda, Rais atazuru Murang’a, na hautakuwa mkusanyiko wa kisiasa. Anakuja
kufungua rasmi masoko yetu yaliyokamilika, kushughulikia masuala ya umeme,
kuboresha barabara zetu, na kukagua miradi inayoendelea ya unyunyizaji maji
mashambani hapa," Kindiki alisema.
Akionekana kumlenga mtangulizi wake aliyebanduliwa Oktoba
mwaka jana, Kindiki alisema kwamba huu si wakati wa kupiga debe za kisiasa bali
ni wakati wa kufanyia wananchi kazi.
Kindiki alifafanua zaidi kwamba kufanya siasa si jukumu la
serikali bali ni jukumu la upinzani.
"Jukumu la serikali sio kutanguliza siasa. Hiyo ni kazi ya
upinzani. Wajibu wa serikali ni kuhakikisha kwamba miradi ya wananchi inafuatiliwa
haraka na kutolewa," aliongeza.
Ruto anatarajiwa kuanza ziara yake rasmi ya kwanza katika
eneo la Mlima Kenya tangu kung’atuliwa ofisini kwa aliyekuwa Naibu Rais,
Rigathi Gachagua, ambaye kwa muda mrefu amejifanya kuwa kinara wa kisiasa wa
eneo hilo.
Tangu kutimuliwa kwa Gachagua, eneo la Mlima Kenya limekuwa
na mgawanyiko mkubwa, huku mrengo mkubwa ambao hapo awali ukimuunga mkono Ruto
kutokana na Gachagua sasa kuhama utiifu wao kwingine.
Mnamo Alhamisi, Machi 20, 2025, Mbunge wa Gatanga Edward
Muriu alionya rais dhidi ya kutaja jina la Gachagua au mapatano yake ya kisiasa
na Raila Odinga katika ziara yake ijayo ya eneo la Mlima Kenya.