
MWANASIASA mkongwe wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye ameripotiwa kumaliza mgomo wake wa kula baada ya kuhamishiwa katika mahakama ya kiraia kutoka mahakama ya kijeshi alikozuiliwa kwa takribani siku 100.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, Besigye amekuwa akisusia
chakula kwa takribani wiki 2, ishara ya kupinga kufunguliwa mashtaka katika
mahakama ya kijeshi sasa amerejelea chakula.
Kiongozi huyo aliwasilishwa katika mahakama ya kiraia mapema
Ijumaa ambapo alifunguliwa mashtaka ya uhaini ambayo adhabu yake ni kifo katika
taifa la Uganda.
Besigye, mgombea urais mara nne katika nchi hiyo ya Afrika
mashariki, alikaa kwenye kiti cha magurudumu alipokuwa akikabiliwa na mashtaka
katika chumba cha mahakama katika mji mkuu, Kampala.
Besigye, 68, amekuwa kizuizini tangu Novemba 16, alipotoweka
katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
Siku kadhaa baadaye, alifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi
mjini Kampala kujibu mashtaka ya kutishia usalama wa taifa.
Mahakama ya Juu ilisimamisha kesi yake ya kijeshi mwezi
uliopita, ikisema jopo la mahakama ya kijeshi haliwezi kuwahukumu raia.
Familia ya Besigye, wafuasi na wengine walitaka aachiliwe
mara moja, lakini aliwekwa katika gereza lenye ulinzi mkali na baadaye kuanza
mgomo wa kula.
Besigye ameonekana kuwa dhaifu katika kufikishwa mahakamani
hivi karibuni, na kusababisha wasiwasi kwamba madhara yoyote kwake jela
yanaweza kusababisha machafuko mabaya. Raia wengi wa Uganda wanazitaka mamlaka
kumwachilia huru kwa misingi ya huruma.
Besigye alirudishwa rumande hadi Machi 7, wakati anatarajiwa
kurejea mahakamani.