
Hatima ya Katibu mkuu
wa ODM Edwin Sifuna iko katika mizani ya kuondolewa au kusalia chamani.
Hii ilitokea baada ya wanachama wa ODM kumsuta wakisema kuwa
kwa muda mrefu ameonekana kupinga sera na maendeleo ya chama.
Mbunge wa Makadara mheshimiwa George Aladwa ambaye pia ndiye
mwenyekiti wa ODM tawi la Nairobi alinukuliwa akimkashifu bwana Sifuna kwa kuwa
na hulka ya kupinga sera za chama na azima ilihali yeye ni katibu mkuu chamani.
Bwana Aladwa katika matamshi yake alidai kuwa bwana Sifuna ni kibaraka wa aliyekuwa naibu wa
rais bwana Rigathi Gachagua na kusema kuwa njama yake ni kuwania kiti cha
Ugavana Nairobi akishirikiana na mheshimiwa Gachagua.
‘’Tunataka kumwambia bwana Sifuna aache kujipiga kifua awaheshimu
viongozi wengine sisi kama viongozi wa ODM tuna heshima, hatutukani viongozi wengine
katika Runinga hata kama ulisoma usitukane wale ambao hawakusoma baadala yake
anzisha kampuni yako ya sheria na uwachane na chama’’ mheshimiwa Aladwa
lieleza.
Chama cha ODM kinaonekana kupasuka Katikati kufuatia kwa
bwana Odinga kupoteza nafasi katika nafasi ya uwenyekiti AUC hivyo kufanya
wanachama Fulani kuunga mkono serikali ya Kenya Kwanza na wengine wakionekana kukosoa
ukuruba kati ya bwana Odinga na Rais Ruto.
Kwa upande mwingine Gavana wa Homabay Gladys Wanga kwa
upande wake alielezea hisia zake akisema kuwa wakati ambapo walikuwa wakihuzunukia
kupoteza ushindi wa AUC wakiwa katika mji wa Addis Ababa nchini Uhabeshi(Ethiopia)
alisema kuwa kulikuwa na Wakenya Fulani kutoka sehemu za nchi walikuwa wakifurahia
kufeli kwa Bwana Odinga.
‘’Wakati ambapo tunalia kule vichochoroni kwa kupoteza
nafasi ya AUC watu wengine wanafurahia, wanacheka na kuinua miguu juu tukasema ni
sawa tu tumejua marafiki zetu ni nani na maadui zetu ni nani’’. Bi Wanga
alisema.
Haya yanapojiri wito wa wanachama wa ODM wanazidi kurai
chama kijitose mzimamzima kwa makubaliano na chama cha Kenya kwanza kwa
kushirikiana.
Siku ya Jumatatu Februari 24,2025 kiongozi wa ODM bwana
Odinga alikutana na Kiongozi wa Taifa Rais William Ruto Katika ikulu ndogo ya
Mombasa ambapo walilakiana na kukaribishwa nyumbani bwana Odinga baada ya kupoteza wadhifa wa
mwenyekiti wa AUC.
Hata hivyo bwana Odinga alikanusha madai kuwa serikali
ilitumia mabilioni ya hela katika kampeni yake,aliahidi kutoa mwelekeo wao kama
chama siku za hivi karibuni.