logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Kwaheri, Mwenyekiti! Ruto amuaga Chebukati, amtambua kama shujaa aliyeweka Kenya mbele

Ruto alimpongeza Chebukati kwa uongozi wake na uthabiti wa tabia, akisema hakuwa mtu wa kutishwa au kushinikizwa.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri09 March 2025 - 10:27

Muhtasari


  •  Ruto alimtaja marehemu Chebukati kama shujaa na mtengeneza historia. Alimsifu kwa ujasiri na uadilifu wake.
  • "Chebukati ameacha urithi wa kipekee wa utumishi bora kwa umma. Kwa heri, Mwenyekiti!" alisema.

Rais William Ruto akizungumza wakati wa mazishi ya Wafula Chebukati mnamo Machi 8, 2025.

Rais William Ruto mnamo siku ya Jumamosi aliwaongoza viongozi wakuu na Wakenya kwa jumla katika kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati.

Chebukati, ambaye alifariki mwezi uliopita baada ya kuugua kwa muda mrefu, alizikwa katika shamba lake lililoko kijiji cha Sabata, eneobunge la Kiminini, kaunti ya Trans Nzoia.

Hafla ya mazishi ilihudhuriwa na viongozi, marafiki, waliowahi kufanya naye kazi, na familia waliokusanyika kumuaga mwanasheria huyo aliyesimamia IEBC kwa miaka sita kabla ya kustaafu mwaka wa 2023.

Katika risala yake baada ya mazishi, Rais Ruto alimtaja marehemu Chebukati kama shujaa na mtengeneza historia. Alimsifu kwa ujasiri na uadilifu wake, akisema kwamba ameacha urithi mkubwa.

 "Mtu mkuu, Wafula Chebukati, amepumzika. Alikuwa mtengeneza historia, mvunja vikwazo, na shujaa wa taifa letu ambaye daima aliweka maslahi ya nchi mbele. Alikuwa jasiri, thabiti, na mwenye maamuzi huru—mwanamume wa uadilifu wa hali ya juu," Ruto alisema kupitia Facebook.

"Mtu mwenye nidhamu na bidii, Chebukati ameacha urithi wa kipekee wa utumishi bora kwa umma. Kwa heri, Mwenyekiti!" aliongeza.

Wakati akihutubia waombolezaji wakati wa mazishi hayo siku ya Jumamosi, Ruto alimpongeza Chebukati kwa uongozi wake na uthabiti wa tabia, akisema hakuwa mtu wa kutishwa au kushinikizwa.

Rais aliongeza kuwa marehemu Chebukati alikuwa chaguo mwafaka kwa nafasi ya mwenyekiti wa IEBC.

"Wakati mwingine watu huambiwa wamepata kazi, lakini kuna wakati kazi humtafuta mtu anayefaa. Na huyo alikuwa Chebukati—kazi ilimpata mwenyewe," Ruto alisema.

Aidha, alimpongeza marehemu kwa kutekeleza majukumu yake ya kikatiba, kisheria, na kiadili kwa umahiri mkubwa alipokuwa akihudumu kama mkuu wa tume ya uchaguzi.

"Katika maisha yake yote, alionyesha uongozi wa hali ya juu na uadilifu mkubwa. Wafula alikuwa mwerevu, jasiri, na mtu wa maadili. Alikuwa shujaa wa taifa letu; hangeweza kupotoshwa kwa sababu alikuwa na akili timamu," Rais Ruto alisema.

 

Ruto pia aliisifu familia ya Chebukati, akimtaja kama baba aliyejitolea kuhakikisha familia yake imelelewa vyema.

 

Rais aliandamana na viongozi mashuhuri akiwemo Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, Spika wa Seneti Amason Kingi, na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, miongoni mwa wengine. Hafla hiyo iligubikwa na hotuba za hisia kali, huku waombolezaji wakitambua mchango wa Chebukati kwa taifa.

 

Chebukati alifariki Februari 20, 2025, katika hospitali moja jijini Nairobi baada ya kupata mshtuko wa moyo. Aligunduliwa kuwa na saratani mwaka wa 2023, miezi michache baada ya kustaafu kutoka IEBC, na alikuwa akipambana na maradhi hayo kwa miaka miwili.


Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved