logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Hofu Uganda baada ya mwanawe Museveni kuwaamuru polisi wampige viboko Bobi Wine na wanachama wake

Muhoozi ametishia kuwa Bobi Wine lazima alazwe hospitalini mwezi huu baada ya kupokea kichapo.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri11 March 2025 - 07:15

Muhtasari


  • Katika moja ya jumbe zake, Muhoozi alitangaza kuwa chama cha NUP kitachukuliwa kama kikundi cha waasi kuanzia Julai 7.
  • "Polisi yeyote atakayekataa kuwapiga wanachama wa NUP atafutwa kazi, bila kujali cheo chake!" alisema. 

Gen Muhoozi Kainerugaba

Kiongozi wa majeshi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amezua mjadala mkali baada ya kutoa vitisho vikali dhidi ya wanachama wa chama cha upinzani cha National Unity Platform (NUP).

Katika mfululizo wa jumbe alizochapisha kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), Muhoozi, ambaye pia ni mwana wa Rais Yoweri Museveni, alitoa maagizo ya moja kwa moja kwa vikosi vya usalama kuwashambulia wafuasi wa NUP.

Kauli zake zimeibua hofu kubwa, huku wakosoaji wakizitaja kuwa ni ishara ya ongezeko la ukandamizaji wa kisiasa nchini Uganda.

Katika moja ya jumbe zake, Muhoozi alitangaza kuwa chama cha NUP kitachukuliwa kama kikundi cha waasi kuanzia Julai 7.

"Baada ya Julai 7, NUP itatangazwa kuwa uasi na vikosi vya usalama vitaruhusiwa kuua yeyote aliye kwenye sare za NUP," aliandika.

Kauli hii, ambayo inampa jeshi mamlaka ya kutumia nguvu kupita kiasi, imeibua taharuki, huku wanaharakati wa haki za binadamu wakihofia kuwa inaweza kutumiwa kama kisingizio cha kushambulia wapinzani wa serikali.

Katika ujumbe mwingine, Muhoozi alitoa amri kali kwa maafisa wa Kikosi Maalum cha Kupambana na Ugaidi (Joint Anti-Terrorism Taskforce - JATT), akisema: "Polisi yeyote atakayekataa kuwapiga wanachama wa NUP atafutwa kazi, bila kujali cheo chake!"

Mwanawe Museveni hakusita kumlenga kiongozi wa NUP, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, akisisitiza kuwa lazima aadhibiwe vikali.

"Mwezi huu wa Machi, JATT lazima impige Kabobi (Bobi Wine). Lazima aende hospitali mwezi huu!" alisema.

Aidha, alitoa maagizo ya moja kwa moja kwa wanajeshi wake kuhakikisha viongozi wengine wa NUP pia wanashambuliwa.

Alimtaja Katibu Mkuu wa chama hicho, David Lewis Rubongoya, akisema: "Nataka JATT impe huyo mwanamke [@DavidLRubongoya] si chini ya viboko 3,000!"

Kauli hizi zimezua taharuki kubwa, huku wengi wakizitafsiri kama ushahidi wa nia ya kuwatisha na kuwaadhibu wapinzani wa Museveni.

Katika ujumbe mwingine, Muhoozi aliamuru mashambulizi dhidi ya yeyote anayevalia mavazi mekundu, rangi inayohusiana na NUP.

"JATT inafanya kazi nzuri, lakini hawapigi wahalifu vya kutosha. Yeyote aliye na sare nyekundu anapaswa kuogopa JATT!" alisema.

Matamshi haya yameibua hasira na ukosoaji mkali kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu na wanasiasa wa upinzani.

"Kauli za Muhoozi ni hatari sana na zinaweza kusababisha mauaji ya wapinzani wa serikali. Tunaitaka jumuiya ya kimataifa kulaani vitendo hivi vya ukandamizaji," alisema mmoja wa wanaharakati wa Uganda.

Chama cha NUP kimeendelea kushinikiza hatua zichukuliwe dhidi ya Muhoozi, kikisema kuwa matamshi yake yanahatarisha maisha ya raia na kuvunja misingi ya demokrasia.

Hadi sasa, serikali ya Uganda haijatoa tamko rasmi kuhusu vitisho hivi, lakini hali ya wasiwasi inaendelea kuongezeka. Wengi wanajiuliza ikiwa haya ni maandalizi ya ukandamizaji mkubwa zaidi wa upinzani kuelekea uchaguzi huo.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved