

Rais William Ruto amejitetea kuhusu kutofika katika eneo la Mlima Kenya kwa miezi sita, akisisitiza kuwa rekodi yake ya maendeleo inajieleza yenyewe.
Akizungumza siku ya Jumatatu usiku, Ruto alipuuza madai kwamba kutokuwepo kwake ni ishara ya kupoteza uungwaji mkono, akisema wakosoaji wake watapata majibu kupitia kazi aliyofanya.
Rais aliongeza kuwa serikali yake imefanikisha miradi muhimu, ambayo ataiwasilisha kwa wananchi wakati wa ziara yake.
“Huenda sijakuwa hapa kwa miezi kadhaa, lakini nina ripoti thabiti kuhusu umeme, nyumba nafuu, masoko na mengi zaidi ambayo nitaonyesha kuanzia kesho (Jumanne),” Ruto alisema katika mahojiano ya moja kwa moja kwenye runinga kabla ya ziara yake.
Rais alikanusha madai kuwa amekuwa akiepuka Mlima Kenya kwa sababu ya uhasama, akisisitiza kuwa anaendelea kutekeleza ahadi zake kwa wakazi wa eneo hilo.
“Nitakaa Mlima Kenya kwa muda mrefu kiasi kwamba watu wataanza kujiuliza kama sina maeneo mengine ya kutembelea,” alisema kwa msisitizo.
Ruto alieleza kuwa ziara yake ya siku tano imepangwa kwa makini na inalenga kuonyesha mafanikio ya serikali yake.
“Huwezi kupima uungwaji mkono wangu kwa msingi wa kutokuwepo kwangu kwa miezi michache. Uhusiano wangu na watu wa Mlima Kenya ni wa kina,” alisema.
Aidha, alikana madai kwamba aliepuka eneo hilo kwa sababu nyingine yoyote, akisema kazi yake itaonyesha ukweli halisi.
“Wanaodai vinginevyo watajionea ukweli wenyewe kesho,” alihitimisha.
Rais William Ruto aliwasili Sagana State Lodge siku ya Jumatatu kabla ya ziara yake ya siku tano ya maendeleo ya Mlima Kenya, itakayoanza leo Aprili 1.
Katika video iliyosambazwa mtandaoni na wanablogu wanaohusishwa na serikali Jumatatu jioni, Rais Ruto alionekana akitangamana na wenyeji kwenye Barabara ya Sagana huku kukiwa na baridi kali.
"Nitakuwa hapa kwa siku tano, mko tayari? Je, mmejitayarisha?" Rais Ruto alisikika akiuliza kundi la vijana waliotafuta hadhira yake alipokuwa akielekea kwenye ikulu ndogo ya Sagana.
Rais pia alimuulizia mchoma mahindi aliyekuwa akiendesha shughuli zake karibu na ikulu ndogo ya Sagana, ambaye rais alisema alimuuzia mahindi ya kuchoma alipozuru Mlima Kenya mwaka 2023.
"Yuko wapi yule mtu aliye na mahindi mazuri ya kuchoma? Nitamuona," Ruto alisema huku wakazi wakimfahamisha kuwa mwanamume huyo yuko karibu.
Kando na kufanya mahojiano, rais pia alikutana na baadhi ya viongozi
waliochaguliwa kutoka eneo la Mt Kenya katika eneo la Sagana State Lodge wakati
wa ziara yake ya siku tano baadaye wiki hii.