logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mwanawe Museveni, Muhoozi Kainerugaba, awapa onyo kali wapenzi wa jinsia moja nchini Uganda

Muhoozi alitangaza kuwa baada ya kunyofoa sehemu za siri, wahusika hao watauawa kwa kukatwa kichwa.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri07 April 2025 - 07:53

Muhtasari


  • Muhoozi alionya kuwa shoga yeyote atakayepatikana ndani ya PLU atakutana na adhabu kali ya kunyofoa sehemu za siri.
  • "Tukimpata shoga yeyote ndani ya PLU, tutamnyoa sehemu za siri katika City Square. Halafu tutamkata kichwa!" alisema.

Muhoozi Kainerugaba

Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mwanawe Rais Yoweri Museveni na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda (UPDF), ametoa onyo kali kwa mashoga nchini Uganda.

Katika taarifa aliyotoa Jumapili jioni, Muhoozi ambaye pia ni Mwenyekiti wa shirika la Patriotic League of Uganda (PLU), alionya kuwa shoga yeyote atakayepatikana ndani ya shirika hilo atakutana na adhabu kali ya kunyofoa sehemu za siri.

Muhoozi aliongeza kuwa baada ya kunyofoa sehemu zao za siri, wahusika hao watauawa kwa kukatwa kichwa.

"Tukimpata shoga yeyote ndani ya PLU, tutamnyoa sehemu za siri katika City Square. Halafu tutamkata kichwa!" alisisitiza Muhoozi.

Patriotic League of Uganda (PLU) ni shirika la kiraia nchini Uganda, lililoanzishwa mapema mwaka 2024 kama sehemu ya mabadiliko ya vuguvugu la MK Movement. Shirika hili linakusudia kukuza uzalendo, fahari ya kitaifa, na uwajibikaji wa raia miongoni mwa wananchi wa Uganda.

Ingawa linashiriki katika masuala ya kitaifa, PLU si chama cha kisiasa. Jenerali Muhoozi amekuwa akiwashauri wanachama wenye malengo ya kisiasa kuungana na chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), akieleza kuwa maadili ya PLU yanalingana kwa karibu na yale ya NRM.

Mwaka mmoja uliopita, Mahakama ya Katiba ya Uganda ilifuta vifungu vinne muhimu vya Sheria ya Kupinga Ushoga ya mwaka 2023. Uamuzi huo ulitolewa na jopo la majaji watano, ambao walitangaza kwamba vifungu vya 3(2)(c), 9, 11(2)(d), na 14 vilikiuka Katiba ya Uganda ya mwaka 1995.

Vifungu vya sheria vilivyofutwa vilikuwa vimeharamisha kukodisha nyumba kwa matumizi ya shughuli za ushoga, kushindwa kuripoti vitendo vya ushoga kwa polisi, na vitendo vya ushoga vinavyosababisha magonjwa hatari kwa watu wengine.

Uamuzi wa Mahakama ulitokana na kesi nne zilizowasilishwa kupinga sheria hiyo, ambayo ilipitishwa na kusainiwa kuwa sheria na Rais Museveni mnamo Mei 26, 2023. Kesi hizo ziliwasilishwa na raia 22 na wanaharakati wa haki za binadamu, waliodai kuwa vifungu vya sheria hiyo vilikiuka haki za binadamu zilizomo katika Katiba ya Uganda na mikataba ya kimataifa kuhusu haki za binadamu.

Hata hivyo, kesi hizo zilipingwa na pande nne, ikiwa ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Family Life Network Limited. Mahakama pia ilipokea ushauri kutoka Shirika la Pamoja la Umoja wa Mataifa kuhusu Ukimwi (UNAIDS) kama amicus curiae (rafiki wa mahakama).

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved